VIONGOZI WA DINI ARUSHA WATOA TAMKO ZITO DHIDI YA UKATILI WA MILA, WALAANI UNYANYASAJI WA WAKRISTO
Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
VIONGOZI wa dini mkoani Arusha, kupitia Umoja wa Kanisa la Arusha (UKAMA), wametoa tamko rasmi na kali kulaani vitendo vya ukatili, udhalilishaji, unyanyasaji wa kijinsia na unyang’anyi wa mali vinavyodaiwa kufanywa kwa kisingizio cha kutetea mila za asili, hususan wakati wa utekelezaji wa masuala ya tohara.
Katika tamko hilo lililotolewa mwanzoni mwa mwaka 2026, UKAMA imesema kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara, vikiambatana na uvunjifu wa amani na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, huku ikidai kuwa baadhi ya wahusika ni waumini wa makanisa lakini bado wanajihusisha na uendeshaji wa ibada za dini za asili kwa misimamo ya kulazimisha.
Kwa mujibu wa waraka huo, watumishi wa Mungu na waumini wao wamekuwa wakikumbwa na vitendo vya kinyama ikiwemo kutekwa nyara, kupigwa, kudhalilishwa hadharani, kuumizwa vibaya wao pamoja na wake zao, hali iliyosababisha baadhi yao kulazimika kuyahama makazi yao kwa kuhofia usalama wao.
Tamko hilo linaeleza kuwa baadhi ya waumini wamelazimishwa kutoa michango na sadaka kwa ajili ya ibada za dini za asili kinyume na imani zao za Kikristo, huku mali zao zikikamatwa au kunyang’anywa wanapokataa. Aidha, waathirika wengine wamedaiwa kupigwa, kumwagiwa mafuta, kutembezwa uchi, kuvalishwa bati na kulazimishwa kutembea umbali mrefu, hali iliyopelekea baadhi yao kulazwa hospitalini kwa matibabu.
UKAMA pia imeeleza masikitiko makubwa juu ya vitendo vya kudhalilisha wanawake, ikiwemo wanawake wajawazito na wagonjwa, ambao hawahusiki na mila hizo lakini wamekuwa wakinyanyaswa na vijana wanaojitambulisha kama “jeshi la mila”. Vijana wasiokubali kujihusisha na ibada za dini za asili nao wamedaiwa kutekwa, kuteswa na kulazimishwa kukana imani zao.
Katika hatua nyingine, viongozi wa kanisa wamesema yapo matukio ya kuvamiwa kwa makanisa na kuharibiwa kwa mali za kanisa, watoto waliokwisha tahiriwa kushikwa na kutahiriwa tena, pamoja na nyumba za waumini kuchomwa moto, hali inayotishia mshikamano na amani ya kijamii.
Uchunguzi wa UKAMA umebaini kuwa asilimia kubwa ya wanaotekeleza vitendo hivyo ni vijana ambao ni waumini wa baadhi ya makanisa, lakini bado wanataka kuendelea kuwa viongozi wa dini za asili, jambo linalosababisha mgongano wa imani na kuilazimisha dini ya asili kutetewa hata kwa kutumia nguvu na umwagaji damu.
“Tunasema wazi kuwa tatizo si tohara, kwa sababu hakuna anayekataa tohara. Tatizo ni ibada na vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika utekelezaji wa tohara hizo,” limeeleza tamko hilo.
Kutokana na hali hiyo, Umoja wa Kanisa la Arusha umetaka waumini wake kuacha mara moja kujihusisha na kuabudu au kulazimisha wengine kushiriki ibada za dini za asili, ukisisitiza kuwa kila Mtanzania ana haki ya kutekeleza tohara kwa ridhaa yake mwenyewe bila kushurutishwa, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, UKAMA imesisitiza kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha tarehe 21 Januari 2010 kuhusu migogoro ya mila yaheshimiwe na pande zote, ili kulinda amani na mshikamano wa wananchi.
Kanisa limeeleza kuwa halitaruhusu dini za asili kuingilia, kufungia au kulitawala Kanisa la Mungu ambalo limesajiliwa kisheria, lina misingi, miongozo, katiba na viongozi wake, huku viongozi wa makanisa wakitakiwa kuwachukulia hatua kali, ikiwemo kuwatenga waumini wanaohusishwa na vitendo hivyo vya uhalifu.
UKAMA imeeleza kuwa vitendo vyote vinavyofanyika vinahesabika kuwa ni makosa ya jinai na yanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ili kuzuia makundi ya kihalifu kujijenga na kuota mizizi ndani ya jamii.
Usainiwaji na Usambazaji wa Waraka
Waraka huo umeandaliwa, kuridhiwa na kusainiwa rasmi na viongozi wakuu wa Umoja wa Kanisa la Arusha (UKAMA), ukiongozwa na Mwenyekiti wa UKAMA, Baba Askofu Dkt. Stanley Hottay (CCT). Pia umesainiwa na Makamu Mwenyekiti wa UKAMA, Mhashamu Baba Askofu Isack Amani (TEC) pamoja na Baba Askofu Dkt. Abel Mollel (CCT) ambaye ni Mdhamini wa Umoja huo.
Vilevile, waraka huo umeungwa mkono na kusainiwa na Baba Askofu Rogers Shemtanbo (CPCT), Mwenyekiti wa UKAMA Mkoa wa Arusha, kama sehemu ya msimamo wa pamoja wa viongozi wa makanisa katika kulinda amani, haki za binadamu na uhuru wa kuabudu.
Nakala za waraka huo zimewasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) pamoja na Mkuu wa Mila wa Malaigwanani, Isack Ole Kisongo Meijo, kwa lengo la kuwashirikisha wadau wa usalama na mila katika kutafuta suluhu ya kudumu na kudhibiti vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kufanywa kwa kisingizio cha mila.
UKAMA imeelekeza kuwa waraka huo usomwe katika makanisa yote ya Arusha ili ujumbe huo uwafikie wananchi wote wanaohusika, kwa lengo la kurejesha amani, mshikamano na kuheshimiana katika jamii.
Ends...

0 Comments