MAZIKO YA MWANASIASA NGULI NA GAVANA WA KWANZA BoT, EDWIN MTEI KUFANYIKA JUMAMOSI NYUMBA KWAKE TENGERU


MAZIKO YA GAVANA WA KWANZA BoT, EDWIN MTEI KUFANYIKA JANUARI 24 TENGERU

Na Joseph Ngilisho – Arushadigital


MAZIKO ya Gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mzee Edwin Mtei (94), yanatarajiwa kufanyika Jumamosi Januari 24, 2026 nyumbani kwake Tengeru, wilayani Arumeru, nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Mzee Mtei alifariki dunia usiku wa kuamkia Januari 19, 2026 mkoani Arusha, baada ya kusumbuliwa na maradhi ya uzee, akiacha historia kubwa katika sekta ya fedha, siasa na harakati za demokrasia nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 20, 2026, mtoto wa marehemu, Melyi Edwin (57), amesema familia imepanga kumzika baba yao katika makaburi ya familia yaliyopo shambani kwake Tengeru.

“Baba amefariki jana usiku. Alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya uzee. Tunatarajia kumzika Jumamosi hapa hapa shambani Tengeru,” amesema Melyi, ambaye ni mtoto wa nne katika familia ya marehemu.

Ameeleza kuwa Mzee Mtei alinunua eneo hilo mwaka 1980 na baada ya kustaafu alijikita zaidi katika kilimo, hususan kilimo cha kahawa, pamoja na shughuli ndogo za kijamii.

“Baba alikuwa mtu mcheshi na mpenda watu. Alipenda kukaa na kila mtu bila ubaguzi. Baada ya kustaafu alikuwa akipenda kuangalia shamba lake la kahawa, lakini kadri umri ulivyokuwa unasonga mbele, alipendelea kukaa nyumbani,” ameongeza Melyi.

CHADEMA YAUNGANA NA FAMILIA KUOMBOLEZA

Katika hatua nyingine, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Tottinani Ndonde, amesema msiba huo umetokea katika kipindi ambacho chama hakikuwa kinatarajia, hususan wakati huu wa maadhimisho ya miaka ya kusajiliwa kwake.

Amesema Mzee Mtei ndiye aliyekabidhiwa cheti cha kwanza cha usajili wa CHADEMA, jambo linalomfanya kuwa alama muhimu katika historia ya chama hicho na demokrasia kwa ujumla.

“Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Mzee Edwin Mtei. Kama CHADEMA, msiba huu unatuhusu moja kwa moja na tutashiriki kwa asilimia 100. Natoa pole kwa wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia wote, kwa kuwa marehemu alikuwa mwasisi na nguzo muhimu ya harakati za demokrasia nchini,” amesema Ndonde.

Ameongeza kuwa chama kimeshafanya mawasiliano na viongozi wa kitaifa na kuazimia kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za msiba na maziko.

“Azimio la chama ni kwamba viongozi wote wa kitaifa, kanda, mikoa na majimbo, pamoja na Bodi ya Wadhamini na wajumbe wote, tutashiriki kwa umoja wetu kuuenzi mchango wa Mzee Mtei,” amesema.

Kwa mujibu wa Ndonde, CHADEMA imepanga kuwa na siku mbili za maadhimisho maalum ya kumuenzi marehemu kabla ya maziko.

“Tunatarajia siku ya Alhamisi na Ijumaa kutakuwa na shughuli rasmi za kichama za kuenzi mchango wake, huku Jumamosi ikiwa ni siku rasmi ya ibada ya maziko na utoaji wa salamu,” ameeleza.

Amesema kilele cha maadhimisho ya kuenzi mchango wa mwasisi huyo kitafanyika Ijumaa, ambapo chama kitatoa salamu rasmi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Amani Golugwa, anatarajiwa kuongoza shughuli zote za uratibu wa maziko hayo kuanzia kesho.

Mara ya mwisho kwa Mzee Edwin Mtei kuonekana hadharani katika shughuli za kijamii ilikuwa mwaka 2021, wakati wa msiba wa mke wake aliyefariki dunia Agosti mwaka huo.

Mzee Mtei anakumbukwa kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa misingi ya uchumi wa taifa na kuanzisha harakati za demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments