Aliyekuwa Gavana wa Kwanza wa BoT na Mwanzilishi wa CHADEMA, Edwin Mtei Afariki Dunia
Na Joseph Ngilisho – ArushaDigital
ALIYEKUWA Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mmoja wa waasisi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mzee Edwin Mtei, amefariki dunia usiku wa kuamkia Januari 19, 2026, akiwa na umri wa miaka 94.
Taarifa za kifo cha kiongozi huyo mkongwe zimethibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche, kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, akieleza kuwa Mtei amefariki akiwa mkoani Arusha.
“Tunasikitika kutangaza kifo cha mzee wetu Edwin Mtei. Tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki. CHADEMA imepoteza nguzo imara na kiongozi mwenye mchango mkubwa kwa chama na taifa kwa ujumla,” ameandika Heche.
Ameongeza kuwa chama hicho kitaendelea kumuenzi Mtei kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika kujenga misingi ya demokrasia, siasa za uwajibikaji na maendeleo ya taifa. “Pumzika kwa amani mzee Mtei,” ameandika Heche.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maandalizi ya mazishi yanaendelea nyumbani kwa marehemu, Tengeru, mkoani Arusha, huku CHADEMA ikitarajiwa kutoa taarifa rasmi zaidi kuhusu ratiba ya mazishi na shughuli za kuaga leo.
Mzee Edwin Mtei anakumbukwa kama mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika historia ya Tanzania, akiwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kuanzishwa kwake, pamoja na kuwahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Kwanza. Baadaye, alijitokeza tena katika ulingo wa siasa za vyama vingi akiwa mmoja wa waasisi wa CHADEMA, chama ambacho kilikuja kuwa miongoni mwa vyama vikuu vya upinzani nchini.
Naye mwanaharakati na Mkurugenzi wa Taasisi ya GH Foundation, Godlisten Malisa, ameungana na Watanzania wengine kutoa salamu za rambirambi, akiandika: “Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Mzee Edwin Mtei na mchango wake mkubwa katika taifa hili. Tumuombee pumziko la amani na kuiombea faraja familia yake.”
Kifo cha Mzee Edwin Mtei kimeacha pengo kubwa katika historia ya uongozi wa kiuchumi na kisiasa nchini, huku wengi wakimtaja kama kiongozi mwenye msimamo, maono na ujasiri wa kusimamia maslahi ya taifa.
Ends

0 Comments