JUKWAA MAALUM ARUSHA LAFUNGUA MILANGO YA MITAJI, MASOKO NA VIVUTIO KWA WAWEKEZAJI WAZAWA

JUKWAA MAALUM ARUSHA LAFUNGUA MILANGO YA MITAJI, MASOKO NA VIVUTIO KWA WAWEKEZAJI WAZAWA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


JUKWAA maalum la uwekezaji lililofanyika mkoani Arusha limefungua ukurasa mpya wa fursa kwa wawekezaji wazawa wadogo na wa kati, baada ya kuwakutanisha na taasisi za kifedha, wadau wa maendeleo pamoja na masoko ya ndani na ya kikanda, kwa lengo la kuinua na kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Jukwaa hilo limeandaliwa na Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA) pamoja na Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC), likiwa na dhamira ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji wa wazawa na kuongeza ushiriki wao katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji na utoaji wa huduma.

Mkutano huo uliwakutanisha wawekezaji kutoka sekta mbalimbali, ukiwalenga kuwajengea uelewa wa kina kuhusu taratibu za kupata mitaji, kutambua fursa za kimkakati zilizopo, pamoja na mbinu bora za kufikia masoko yenye ushindani ndani na nje ya nchi.

Akitoa mada kuhusu mazingira ya uwekezaji nchini, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, aliwahimiza wawekezaji kusajili miradi yao rasmi ili kunufaika na hadhi ya uwekezaji unaotambuliwa kisheria. Alieleza kuwa usajili huo unawawezesha wawekezaji kupata Vyeti vya Uwekezaji vinavyotoa ulinzi wa kisheria na kufungua milango ya vivutio mbalimbali vya Serikali.


Alibainisha kuwa vivutio hivyo ni pamoja na msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa forodha kwa mashine na vifaa vya uzalishaji, hatua inayolenga kupunguza gharama za kuanzisha na kuendesha miradi ya uwekezaji, hususan kwa wazawa.

Kwa upande wa mitaji, Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) ilieleza kuwa imejipanga kikamilifu kuwa mshirika wa karibu wa wawekezaji wazawa, hasa wa ngazi ya kati na ndogo, kupitia bidhaa za mikopo zilizobuniwa mahsusi kuchochea maendeleo ya miradi ya uzalishaji.


Akizungumza kwa niaba ya benki hiyo, Mkurugenzi wa Mipango wa TIB, Joseph Felix Chilambo, alisema dhamira ya benki ni kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyokwamisha jitihada za Watanzania kuwekeza katika viwanda na biashara zinazoongeza thamani ya malighafi za ndani.


Rais wa TNCC, Vicent Minja, alisema chemba hiyo itaendelea kuwa daraja muhimu kati ya wawekezaji wazawa na masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa, akisisitiza kuwa upatikanaji wa masoko ni nguzo kuu ya uendelevu wa uwekezaji na ukuaji wa biashara.

Aliongeza kuwa kupitia mtandao mpana wa TNCC ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara wa ndani wana fursa ya kupata washirika wa kimkakati, kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za biashara na kufungua masoko mapya yatakayoongeza ushindani na ubora wa bidhaa za Tanzania.

Naye Afisa Mtendaji wa EABC, Iman Kajula, alisema jukwaa hilo limekuwa chachu muhimu ya kuwajengea wawekezaji wazawa ujasiri na uelewa mpana wa fursa zilizopo katika ukanda wa Afrika Mashariki na nje ya mipaka ya nchi.

Alisema mkutano huo umewezesha majadiliano ya ana kwa ana kati ya wafanyabiashara na wadau wa maendeleo, hatua iliyowasaidia wawekezaji kujifunza kutoka uzoefu wa wengine na kufanya maamuzi ya kimkakati ya kupanua au kuanzisha uwekezaji wenye tija.

Jukwaa hilo limefanikiwa kufanyika kwa udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ikiwa ni sehemu ya jitihada za pamoja za kuimarisha uwekezaji wa wazawa na kukuza uchumi wa taifa.




Ends..

Post a Comment

0 Comments