MAJONZI NA VILIO YATAWALA MAZIKO YA WATOTO WAWILI WALIOKUFA MAJI WAKIOGELEA HOTELINI ,MBUNGE ATOA POLE KWA FAMILIA ATAKA WAZAZI KUWEKA ULINZI WA WATOTO,VIONGOZI WATAKA KIBANO KWA WAMILIKI WA HOTELI KWA UZEMBE.

MAJONZI YATAWALA MAZIKO YA WATOTO WAWILI WALIOFARIKI KWA KUZAMA ARUSHA, WANANCHI WATAKA HATUA KALI DHIDI YA UZEMBE

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU

 


HUZUNI, vilio na majonzi makubwa vimetawala wakati wa ibada ya mazishi ya watoto wawili wa familia moja, Abednego Joachim (13) na Ebenezer Joachim (9), waliopoteza maisha kwa kuzama maji walipokuwa wakiogelea katika bwawa la kuogelea (swimming pool) lililopo kwenye hoteli moja eneo la Sakina, Jijini Arusha.


Ibada hiyo ya mazishi, iliyofanyika nyumbani kwa familia  na kufuatiwa na maziko nyumbani kwa marehemu katika kijiji na kata ya Kimnyaki, wilayani Arumeru, ilihudhuriwa na maelfu ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa serikali, vyama vya siasa, taasisi za dini pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali. 


Baadhi ya waombolezaji walishindwa kujizuia na kuzimia kutokana na uzito wa tukio hilo la kusikitisha.

Waombolezaji wameeleza masikitiko yao makubwa, wakilitaja tukio hilo kuwa limetokana na uzembe wa wamiliki wa hoteli, na kuitaka serikali kuchukua hatua kali za kisheria ili kukomesha matukio ya aina hiyo yanayohatarisha maisha ya watoto na wananchi kwa ujumla.


Akitoa salamu za rambirambi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC), Baraka Simion, alisema vifo vya watoto hao vimeacha pengo kubwa kwa familia na jamii kwa ujumla, huku ndoto zao zikikatizwa ghafla.


 Alieleza kuwa mtoto mmoja alikuwa anatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari, huku mwingine akiendelea na masomo ya shule ya msingi.


Mwenyekiti huyo alizitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika, akisisitiza kuwa uzembe wa aina hiyo haupaswi kuvumiliwa. 


Aidha, aliagiza mamlaka husika kusitisha kwa muda huduma za uogeleaji katika hoteli husika hadi uchunguzi utakapokamilika ili kubaini kama eneo hilo lina sifa za kuendelea kutoa huduma hiyo.


Pia alitoa wito kwa mamlaka zinazohusika kufanya tathmini ya kina kwa hoteli zote zenye mabwawa ya kuogelea, ili kuhakikisha zinazingatia viwango na masharti ya usalama kabla ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.


Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, alitoa pole kwa familia ya marehemu na kuwataka wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wao, hasa wakati wa shughuli za starehe kama kuogelea. 


Dkt. Lukumay, ambaye alipewa heshima ya kuweka shada la maua kwenye makaburi ya pamoja ya marehemu, alisema ulinzi wa watoto ni jukumu la kila mzazi na jamii kwa ujumla.


Naye Askofu wa Kanisa la Baptisti, Samweli Mollel, aliyeongoza ibada ya mazishi, aliwataka wananchi kuacha kuhusisha tukio hilo na imani potofu, ikiwemo madai ya kafara.


 Alisisitiza kuwa ni vyema jamii ikaelekeza nguvu zake katika kuelimishana juu ya usalama wa watoto badala ya kusambaza dhana zisizo na msingi.


Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Halmashauri ya Arusha, Nicholas Sawa, alisema Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na tukio hilo na kimetoa pole kwa familia iliyofiwa, akiwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.












Ends..


Post a Comment

0 Comments