DUKA LA “MAMBO LEO” LAUNGUA MOTO ARUSHA, HASARA KUBWA YARIPOTIWA
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Moto huo ulizuka majira ya saa moja usiku muda mfupi baada ya duka kufungwa saa kumi na mbili jioni, na uliendelea kuwaka kwa zaidi ya masaa sita, hali iliyozua taharuki, mshangao na masikitiko makubwa miongoni mwa wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo. Mashuhuda walisema moshi mzito pamoja na harufu kali ya bidhaa zinazoungua vilitanda, huku wananchi wakihamaki na kukimbia hovyo kutokana na hofu.
Duka hilo lilikuwa limejaa bidhaa mbalimbali za umeme zikiwemo televisheni, redio, friji, taa, betri za simu, nyaya (cables), kamera na vifaa vingine vya majumbani, vyote vikiteketea kwa moto.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jiji la Arusha, Oswald Mwanjegele, alisema jeshi hilo lilipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa mbili usiku na kufika eneo la tukio kwa ajili ya uokoaji.
“Tulipofika tulikumbana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa njia za kupenya ndani ya jengo. Njia zote za uokozi zilikuwa zimezibwa kutokana na wafanyabiashara kuweka stoo za bidhaa hadi juu ya bati, hali iliyofanya zoezi la kuzima moto kuwa gumu sana,” alisema Mwanjegele.
Aliongeza kuwa, licha ya changamoto hizo, jeshi la zimamoto lilifanikiwa kudhibiti moto na kuzuia usisambae kwenye majengo jirani. Hata hivyo, alionya kuwa kitendo cha kuziba njia za upenyo na vichochoro kwa kuhifadhi bidhaa ni hatari kubwa kwa usalama, hususan wakati wa majanga.
“Tulichobaini ni kuwa eneo hilo halikutumika tena kama sehemu ya biashara pekee, bali pia kama stoo zisizo na mpangilio. Njia zote za uokozi zilikuwa zimezibwa, jambo ambalo ni hatari sana,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Jeshi la Zimamoto, hakuna madhara ya kibinadamu yaliyoripotiwa katika tukio hilo. Chanzo cha moto bado hakijafahamika, huku uchunguzi ukiendelea kubaini kilichosababisha janga hilo.
Mwanjegele pia alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuimarisha ulinzi katika eneo la tukio, akieleza kuwa kulikuwa na viashiria vya vibaka kujaribu kuchukua mali, lakini walidhibitiwa mapema.
"Wakati tuna zima moto tumekumba na changamoto nyingi sana Kuna mfanyabiashara anastoo ya bidhaa na alikiwa hataki kufungua alikuwa tayari hata bidhaa ziungulie ndani sijui amefungia nini hii ni hatari sana"Alisema Mwanjegele
Kwa upande wake, mmiliki wa duka hilo, Vitalis Timira (Mambo Leo), hakuwa tayari kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana na tukio hilo hadi muda wa taarifa hii inachapishwa.
Tukio hilo limeacha funzo kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuweka miundombinu rafiki kwa uokoaji, pamoja na kuzingatia kanuni za usalama ili kuepusha madhara makubwa zaidi endapo majanga yatatokea.
Ends..





0 Comments