Na Joseph Ngilisho – ARUMERU
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amempongeza Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, kwa kutembelea k eneo la Ngaramtoni na kuangalia mradi mkubwa wa barabara ya Mianzini -Timbolo na Ngaramtoni unaotekelezwa kwa gharama ya sh,bilioni 23 katika jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,januari 11,2025 Dkt. Lukumay alisema kuwa wananchi wa Arumeru Magharibi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa za miundombinu ya barabara, hususan barabara za vijijini ambazo hazipitiki, na zile chache zilizopo zikiwa na uharibifu mkubwa.
“Tunashukuru sana kwamba Naibu Waziri ametembelea barabara ya Miyanzini – Ngaramtoni. Barabara hii ni ya umuhimu mkubwa kwani itarahisisha usafiri wa wananchi na kuboresha uchumi wa eneo letu. Kwa muda mrefu wananchi wa vijiji zaidi ya 35 wamekosa barabara zinazopitika, na hii ziara inaleta matumaini makubwa,” alisema Dkt. Lukumay.
Mbunge huyo alibainisha kuwa mradi wa barabara ya Mianzini unakamilika ndani ya miezi sita hadi saba, lakini bado kuna kipande cha barabara cha kilomita 5.1 kuanzia Sambasha hadi Ngaramtoni ambacho hakijaingizwa kwenye bajeti ya utekelezaji. Dkt. Lukumay aliomba kwa heshima kuhakikisha kipande hiki kizingatiwe ili wananchi wapate barabara kamili na ya kiwango cha lami.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa miradi mingine ya barabara ikiwemo ya Mbauda–Oljoro–Losunyai na Malala–Mlangarin–Nduruma–mpaka Bwawani, ambapo wananchi wanateseka kutokana na hali mbaya ya barabara.
“Kukamilika kwa miradi hii kutawawezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi, kuongeza shughuli za kibiashara, na kuimarisha uchumi wa jimbo letu,” alisema Dkt. Lukumay.
Mbunge huyo pia aliishukuru serikali kwa jitihada za kuweka mitaro ya maji katika barabara za vijijini, hatua inayosaidia kudhibiti mmomonyoko wa ardhi na mafuriko, hasa katika milima na maeneo ya Olmotoni na Ngaramtoni.
Ziara ya Naibu Waziri Kasekenya ilichangia matumaini makubwa kwa wananchi wa Arumeru Magharibi ambao kwa miaka mingi wamekabiliwa na changamoto za miundombinu.
Dkt. Lukumay aliishukuru serikali kwa mradi wa barabara unaoendelea na kuahidi kushirikiana ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri.
“Tuna imani kuwa barabara hizi zitakapokamilika, zitabadilisha maisha ya wananchi, zitaimarisha biashara na uchumi, na kuleta maendeleo ya kweli katika jimbo letu,” alimalizia Mbunge Lukumay.
Ends..












0 Comments