KWAGILWA AAGIZA MIFUMO YA KIDIGITALI NA NISHATI SAFI KATIKA SHULE MAALUM ZA SAYANSI,ATOA MAAGIZO MAZITO SHULE YA SAMIA GIRLS LONGIDO

KWAGILWA AAGIZA MIFUMO YA KIDIGITALI NA NISHATI SAFI KATIKA SHULE MAALUM ZA SAYANSI

Na Joseph Ngilisho – LONGIDO

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu), Reuben Kwagilwa, ameagiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka na madhubuti ili kuhakikisha shule zote mpya za sekondari maalum zenye mchepuo wa Sayansi nchini zinafungwa mifumo ya kisasa ya ufundishaji kwa njia ya kidigitali (e-learning).

 Alisisitiza kuwa matumizi ya TEHAMA si hiari bali ni hitaji la msingi katika elimu ya kisasa.

Kwagilwa alieleza kuwa mifumo hiyo ya kidigitali ni mhimili muhimu wa mageuzi ya elimu ya Sayansi na Teknolojia, sambamba na kuwa suluhisho la kudumu dhidi ya changamoto ya uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi, hususan katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa rasilimali watu.



Agizo hilo  wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua mazingira ya ufundishaji na miundombinu ya elimu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Longido Samia Girls, wilayani Longido, mkoani Arusha. 

Shule hiyo ni miongoni mwa shule 26 mpya maalum za Sayansi zilizojengwa nchini kote, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).


Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri alisema matumizi ya mifumo ya e-learning yataongeza ubora na ufanisi wa ufundishaji kwa kuwezesha mbinu shirikishi za kujifunza, kuongeza uelewa wa wanafunzi na hatimaye kuinua viwango vya ufaulu katika masomo ya Sayansi.

Alifafanua kuwa Serikali, kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali cha Hombolo, imejipanga kuhakikisha miundombinu ya kidigitali inafungwa, inasimamiwa na inatumika ipasavyo katika shule zote maalum za Sayansi ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

“Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna mwanafunzi wa Sayansi anayenyimwa elimu bora kwa kisingizio cha uhaba wa walimu. Kupitia TEHAMA, ufundishaji utaendelea kwa ufanisi na kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa,” alisema Kwagilwa kwa msisitizo.


Katika hatua nyingine, Naibu Waziri ameagiza matumizi ya lazima ya nishati safi katika shule zote mpya za sekondari maalum, akibainisha kuwa Serikali tayari imekamilisha ufungaji wa miundombinu ya nishati safi katika shule hizo kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya uhifadhi wa mazingira.


Aliweka marufuku kali dhidi ya matumizi ya kuni na mkaa katika shule zote zilizounganishwa na nishati safi, akisisitiza kuwa ukiukwaji wa agizo hilo hautavumiliwa.


 “Ni marufuku kabisa kutumia kuni au mkaa katika shule zilizounganishwa na nishati safi. Hili ni agizo la Serikali na ni utekelezaji wa moja kwa moja wa ajenda ya kitaifa ya matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira,” alisisitiza.


Aidha, Kwagilwa aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kusimamia kwa karibu na kwa uwajibikaji wa hali ya juu zoezi la uandikishaji na uripoti wa wanafunzi wa darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza, akielekeza hatua za haraka zichukuliwe kwa wanafunzi ambao hawajaripoti ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitatua mapema.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alishuhudia wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Longido Samia Girls wakifanya majaribio ya kisayansi katika somo la Baiolojia, ambapo aliwapongeza kwa umahiri wao wa kutumia vifaa vya maabara na kuonesha uelewa wa kina wa mafunzo kwa vitendo.


Wanafunzi hao walieleza kuwa mafunzo ya vitendo yamekuwa yakiwajengea uwezo mkubwa wa kuelewa na kukumbuka masomo kuliko kujifunza kwa nadharia pekee, hali inayochangia kuimarika kwa ufaulu wao katika masomo ya Sayansi.


Kwagilwa aliwapongeza wanafunzi hao na kuwasisitiza kusoma kwa bidii, akibainisha kuwa Serikali imejenga shule hiyo kwa lengo la kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora katika mazingira rafiki, salama na yenye vifaa vyote muhimu vya kujifunzia na kufundishia.


Alibainisha kuwa ujenzi wa shule maalum za wasichana zinazotoa mchepuo wa Sayansi unalenga kubadili mtazamo hasi uliokuwepo awali kuwa masomo ya Sayansi ni ya wavulana, na badala yake kuwapa wasichana fursa sawa ya kushiriki na kufanikiwa katika taaluma hizo.


“Ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuwawezesha wasichana. Ujenzi wa shule 26 maalum za wasichana nchini ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora, hususan katika masomo ya Sayansi,” alisema Mhe. Kwagilwa.


Aidha, kufuatia ombi la Mbunge wa Longido na Naibu Waziri wa Mifugo kuhusu kuwapa fursa watoto wa Longido kujiunga na shule hiyo, Kwagilwa alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha kuona namna ya kuongeza idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaopangiwa shule hiyo, kwa kuwachukua wasichana wenye ufaulu mzuri kutoka wilaya ya Longido, licha ya shule hiyo kuwa ya kitaifa.






Mwisho.

Post a Comment

0 Comments