TARURA YAHIMIZA UTEKELEZAJI MIRADI YA BARABARA MERU, TENGERU–NAMBALA YAWEKWA LAMI

TARURA YAHIMIZA UTEKELEZAJI MIRADI YA BARABARA MERU, TENGERU–NAMBALA YAWEKWA LAMI

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU


MENEJA wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Nicholas Francis, amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru.

Akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu), Reuben Kwigilwa, ya kukagua utekelezaji wa miradi ya barabara, Mhandisi Francis alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Tengeru–Nambala unaotekelezwa kwa kiwango cha lami ni ushahidi wa dhamira ya Serikali kuboresha usafiri na usalama wa wananchi.

Alifafanua kuwa barabara ya Tengeru–Nambala ina jumla ya urefu wa kilomita 3.8, ambapo awamu ya kwanza ya kilomita 0.5 inajengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Mfuko wa Barabara (Road Fund Development). Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya M/S Rocktonic Ltd kwa gharama ya Sh milioni 699, na ulianza rasmi tarehe 14 Julai 2025 huku ukitarajiwa kukamilika Machi 11, 2026.

Kwa mujibu wa Meneja huyo wa TARURA, hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 66.4, ambapo kazi kuu zilizokamilika ni pamoja na kusafisha eneo la mradi, kukata na kujaza barabara kufikia levo stahiki, kuweka tabaka la kwanza na la pili la changarawe (G15 na G45), kuweka tabaka la kokoto kwa urefu wa mita 500, pamoja na ujenzi wa mitaro ya maji yenye urefu wa mita 800.


Aidha, alisema mradi umehusisha ujenzi wa vivuko 132, kalvati moja la zege jiwe, pamoja na eneo la watembea kwa miguu lenye urefu wa mita 1,000, hatua inayolenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara hususan wanafunzi na wakazi wa maeneo jirani.

Katika upande wa malipo, Mhandisi Francis alieleza kuwa hadi sasa mkandarasi amelipwa kiasi cha Sh milioni 185.6 sawa na asilimia 26 ya thamani ya mradi, huku TARURA ikiendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inaonekana.

Hata hivyo, alisema mradi huo umekumbana na changamoto ya upungufu wa lami nchini, hali iliyosababisha kupanda kwa gharama ya malighafi hiyo muhimu. Aliongeza kuwa hatua tayari zimechukuliwa kutatua changamoto hiyo, ambapo mkandarasi ameagiza lami na tayari imewasili bandarini, na taratibu za mwisho za kuitoa zinaendelea ili kazi za mwisho zikamilike kwa wakati uliopangwa.

Mhandisi Francis alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara inayogusa maisha ya wananchi wa Meru. Vilevile alimpongeza Naibu Waziri Kwigilwa kwa ziara yake ya kukagua na kutoa maelekezo yatakayoharakisha ukamilishaji wa mradi huo muhimu.

Ziara hiyo ilionyesha msisitizo wa Serikali katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa karibu, kuhakikisha inakamilika kwa viwango vilivyokusudiwa na kuleta tija kwa wananchi.

Ends.

Post a Comment

0 Comments