FIFA YACHUKIA FUJO FAINALI MOROCCO, CAF YAMSUBIRI KOCHA SENEGAL ADHABU NZITO
By Arushadigital
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amelaani vikali matukio ya utovu wa nidhamu yaliyojitokeza katika mchezo wa fainali uliochezwa nchini Morocco, akisisitiza kuwa vurugu pamoja na hatua ya kuondoka uwanjani ni kinyume kabisa na misingi ya soka la kisasa.
Katika taarifa rasmi aliyoitoa kwa Shirika la Habari la AFP, Infantino alisema FIFA haiwezi kuvumilia vitendo vinavyoharibu taswira ya mchezo huo pendwa duniani. “Tunalaani vikali tabia ya baadhi ya ‘mashabiki’, wachezaji na baadhi ya benchi la ufundi la Senegal. Haikubaliki kabisa kuacha uwanja wa michezo kwa namna ile, na vurugu hazina nafasi katika mchezo wetu,” alisema Infantino kwa msisitizo mkubwa.
Pamoja na lawama hizo, Rais huyo wa FIFA alitumia fursa hiyo kuipongeza Morocco kwa maandalizi na uandaaji wa hali ya juu wa mashindano hayo, akibainisha kuwa tukio hilo limekuwa jaribio muhimu kuelekea maandalizi ya taifa hilo kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2030. Alisisitiza kuwa Morocco imeonesha uwezo mkubwa wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Morocco, Walid Regragui, hakuficha masikitiko yake juu ya taswira mbaya iliyojitokeza, akieleza kuwa matukio ya fainali hiyo yameliacha soka la Afrika katika hali ya aibu mbele ya macho ya dunia. “Taswira tuliyotoa kuhusu soka la Afrika haikubaliki kabisa. Kusimamishwa kwa mchezo kwa zaidi ya dakika 10 wakati dunia nzima ikiutazama ni jambo la kusikitisha sana,” alisema Regragui.
Kauli ya Regragui inaakisi hofu ya wadau wengi wa soka barani Afrika kuwa vitendo vya aina hiyo vinaweza kudhoofisha jitihada zinazofanywa kwa miaka mingi kuinua hadhi na heshima ya soka la Afrika katika ramani ya kimataifa.
Wakati huo huo, sakata hilo limeingia katika mikono ya Tume ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ambayo inatarajiwa kuchukua hatua kali dhidi ya Kocha wa Senegal, Pape Thiaw, kwa kuhusika moja kwa moja na uamuzi wa kuiondoa timu uwanjani. Vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa adhabu hiyo huenda ikawa ya muda mrefu ili kutoa funzo kwa wahusika wengine.
Hatua hiyo inaungwa mkono na msimamo thabiti wa Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, ambaye amekuwa akisisitiza mara kwa mara umuhimu wa nidhamu na kulinda heshima ya soka la Afrika. “Tunaendesha soka la Afrika kwa ajili ya Waafrika,” amekuwa akikariri Motsepe, akionesha dhamira ya dhati ya kuona mchezo huo ukiongozwa kwa misingi ya haki, nidhamu na ushindani wa kweli.
Ingawa idadi kamili ya mechi ambazo kocha Thiaw atazuiliwa bado haijawekwa wazi, wachambuzi wa soka wanaamini kuwa adhabu hiyo itakuwa ujumbe mzito kwa makocha, wachezaji na viongozi wote kuwa vitendo vya migomo na vurugu havina nafasi tena katika soka la kisasa barani Afrika.

0 Comments