BIMA YA AFYA KWA WOTE YAIVA RASMI KUANZA JANUARI 26, 2026


BIMA YA AFYA KWA WOTE YAIVA RASMI KUANZA  JANUARI 26, 2026

Na Arushadigital – Dodoma

Baada ya miaka ya ahadi, maandalizi, mipango na mikakati ya kina, Watanzania wanatarajiwa kuanza kunufaika rasmi na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (BAW), hatua itakayoweka historia mpya katika sekta ya afya nchini. Mpango huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi kuanzia Jumatatu, Januari 26, 2026, kwa awamu ya kwanza, ukiwa na lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila kikwazo cha kifedha.

Kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu kunatekeleza moja kwa moja ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, ambapo aliahidi kuwa ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa, Serikali yake ingeanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kama nguzo muhimu ya ustawi wa wananchi.

Kupitia mpango huo, Serikali inatarajia kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi wasio na uwezo, wakiwemo wazee, watoto, wanawake wajawazito na watu wenye ulemavu. Makundi hayo yameainishwa kuwa ya kipaumbele, huku gharama zao za matibabu zikitarajiwa kubebwa na Serikali ili kuwawezesha kupata huduma bora za afya kwa wakati na kwa heshima.

Taarifa rasmi kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo imetolewa leo Ijumaa, Januari 23, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati wa kikao kazi cha kitaifa cha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, kilichowakutanisha viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya afya na wawakilishi wa skimu za bima.

Waziri Mchengerwa amesema awamu ya kwanza ya utekelezaji itahusisha kuanza kutumika kwa kitita cha huduma muhimu, kitakachotolewa kupitia skimu za bima ya afya zilizopo, kikilenga zaidi makundi yaliyo hatarini, ili kuhakikisha yanapata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.

Amefafanua kuwa gharama ya kitita hicho ni Shilingi 150,000 kwa kaya isiyozidi watu sita, huku huduma zitakazotolewa zikiendana na utaratibu wa rufaa katika vituo vya afya na hospitali zilizoingia mkataba rasmi na skimu za bima ya afya.

“Bima ya Afya kwa Wote si mradi wa wizara moja wala mpango wa muda mfupi. Ni ahadi ya Taifa kwa wananchi wake. Mafanikio ya mpango huu hayatapimwa kwa hotuba au maagizo, bali kwa idadi ya wananchi wanaolindwa dhidi ya gharama kubwa za matibabu na wanaopata huduma za afya kwa heshima na usawa,” amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kubeba dhamana ya moja kwa moja, binafsi na isiyohamishwa ya kusimamia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote katika mikoa yao, akisisitiza kuwa usimamizi thabiti ngazi ya mikoa na halmashauri ndio msingi wa mafanikio ya mpango huo.

Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatajwa kuwa miongoni mwa mageuzi makubwa ya kijamii yanayolenga kuimarisha usawa wa upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza umaskini unaotokana na gharama za matibabu na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa kwa ujumla.

Ends..

Post a Comment

0 Comments