WATANO WAJERUHIWA KWA MAPANGA KATIKA VURUGU ZA KUGOMBEA MPAKA WA VIJIJI NGORONGORO.

  WATANO WAJERUHIWA KATIKA VURUGU ZA KUGOMBEA MPAKA WA VIJIJI NGORONGORO,DC ATAJWA.

Na Joseph Ngilisho-NGORONGORO.

WAKAZI watano wa Kijiji cha Orukuyene, Kata ya Oloipiri, Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro, wamejeruhiwa kwa mapanga baada ya kuzuka kwa vurugu kali zilizohusisha matumizi ya mapanga, marungu na fimbo, kufuatia mvutano wa muda mrefu wa mpaka wa vijiji kati ya Orukuyene (Kata ya Oloipiri) na Lopoluni (Kata ya Olorien Magaiduru), Tarafa ya Loliondo.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Orukuyene, Terat Sindai Sakaja, alisema tukio hilo lilitokea jana Januari 22, 2026, majira ya mchana, wakati Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,  Huseni, alipokuwa akionesha alama (vibao) vya mipaka ya vijiji husika katika eneo la Kitongoji cha Engutoto upande wa Orukuyene na Kitongoji cha Olobo upande wa Lopoluni.



Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, zoezi hilo liligeuka kuwa vurugu baada ya pande husika kutofautiana juu ya uhalali wa mipaka iliyooneshwa.


Alitaja majeruhi kuwa ni Kasosi Puroka (Mwenyekiti wa Kitongoji cha Engutoto), Saning’o Minisi, Kelembu Shuputu, Kadogo Partumar na Njojo Shiria. 


Alisema wote wamekimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya Wasso ambako wanaendelea kupatiwa matibabu, huku hali zao zikielezwa kuwa zinaimarika.


Katika kuendelea kwa tukio hilo, baadhi ya wadau na wananchi wameelekeza lawama zao kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Brigedia Jenerali Wilson Christian Sakulo, wakidai kucheleweshwa kwa ugawaji wa vyeti na ramani za mipaka ya vijiji ndiko kunakochochea migogoro ya ardhi wilayani humo. 


Wadau hao walisema mpango wa upimaji, uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi na utoaji wa vitabu vya mipango ya matumizi ya ardhi ulikamilika tangu mwaka 2022, na kwamba Halmashauri ilikuwa imepanga kugawa nyaraka hizo mwezi Februari 2025, lakini zoezi hilo lilisimamishwa.


“Msingi wa migogoro hii ni kukwama kwa ugawaji wa vyeti na vitabu vya mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji. Nyaraka hizo zingebainisha wazi mipaka ya vijiji na kuondoa sintofahamu. Kuchelewa huko kumezaa migogoro mfululizo,” alisema mwananchi mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake, akiongeza kuwa migogoro iliyotokea awali ni kati ya Kritalo na Oloipiri, Maaloni na Yasimdito, Sale na Yasimdito, na sasa Orukuyene na Lopoluni.


Hata hivyo, kutokana na uzito wa tuhuma hizo, mamlaka za wilaya zimeombwa kutoa ufafanuzi wa kina na kuchukua hatua za haraka ili kuzuia migogoro zaidi, ikiwemo kuhakikisha nyaraka za mipaka ya vijiji zinapatikana kwa wakati na kwa uwazi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,  Murtalah Sadiq Mbillu, alisema kwa njia ya simu kuwa alikuwa nje ya wilaya kikazi wakati tukio linatokea na hakuwa amepata taarifa za awali juu ya chanzo cha vurugu hizo.


 Hata hivyo, amekiri kuwa Halmashauri ilipanga kugawa vyeti na vitabu vya mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji mwezi Februari mwaka jana, lakini zoezi hilo halikufanyika kwa wakati uliopangwa.


 Aliongeza kuwa tayari taarifa zimeshatolewa kwa Watendaji wa Vijiji kufika Halmashauri kuchukua vyeti hivyo.


Wadau wa ardhi na amani wilayani Ngorongoro wameendelea kusisitiza umuhimu wa uratibu wa karibu kati ya Serikali, viongozi wa vijiji na wananchi, pamoja na utekelezaji wa haraka wa mipango ya ardhi, ili kudhibiti migogoro inayohatarisha usalama wa wananchi na mali zao.


Ends..

Post a Comment

0 Comments