MERU YAMUOMBEA MZEE MTEI, YASEMA TAIFA LIMEPOTEZA NGUZO MUHIMU
Na Joseph Ngilisho-ARUMERU
HALMASHAURI ya Wilaya ya Meru imesema imepatwa na msiba mkubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mzee Edwin Mtei, ikieleza kuwa taifa limepoteza kiongozi mahiri aliyeitumikia Tanzania kwa uadilifu, weledi na kujitoa.
Akizungumza wakati wa kutoa pole nyumbani kwa marehemu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Lucas Kaaya, alisema Meru imeguswa kwa namna ya kipekee na msiba huo kutokana na mchango mkubwa wa marehemu kwa taifa pamoja na uamuzi wake wa kuishi na kuzikwa Meru.Kaaya alisema taarifa za msiba huo zimepokelewa kwa huzuni kubwa, akibainisha kuwa mzee Mtei alikuwa mtu wa watu, mwenye historia nzito ya kulitumikia taifa katika nafasi mbalimbali muhimu.
“Tumepokea taarifa hizi kwa huzuni kubwa. Msiba huu ni mzito kwa sababu ya namna mzee Mtei alivyoishi na watu, lakini pia kwa mchango wake mkubwa kwa Tanzania. Kama Halmashauri ya Meru tumeona ni wajibu wetu kufika, kuungana na wafiwa na kutoa pole kwa dhati kabisa,” alisema Kaaya.
Alisema marehemu alikuwa mwana Meru halisi, aliyeamua kuishi Meru hadi mwisho wa maisha yake na pia kuchagua kuzikwa katika ardhi hiyo, jambo lililoipa Meru heshima ya kipekee kuwa sehemu ya historia yake.
Mwenyekiti huyo alikumbusha kuwa mzee Mtei alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, nafasi aliyotumia kuweka misingi imara ya sera za fedha nchini, pamoja na kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha mifumo ya kifedha na ushauri wa kitaalamu.
“Mzee Mtei alikuwa mtaalamu mbobevu wa masuala ya fedha. Amehusika katika kuunda sera muhimu za kifedha, kutoa ushauri kwa taasisi mbalimbali, na kusaidia maendeleo ya elimu hasa katika maeneo yanayohusiana na masuala ya fedha,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Kaaya, msiba wa mzee Mtei si wa Meru pekee bali ni wa Tanzania nzima, akisisitiza kuwa mchango wa marehemu unatambulika kitaifa na kimataifa.
“Huu ni msiba wa Watanzania wote. Tumefiwa na mtu maarufu, mtu aliyelitumikia taifa hili kwa nguvu na jasho. Kama Meru tumeamua kuungana kwa pamoja, kulia na familia na kushiriki majonzi yao,” alisema.
Akihitimisha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru aliwapa pole familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mtei, akisisitiza kuwa Meru itaendelea kuenzi na kuthamini mchango wake kwa maendeleo ya taifa.
Ends..







0 Comments