TRA ARUSHA YAZIDI KUPATA MAFANIKIO KWA KUIMARISHA UKUSANYAJI WA MAPATO-RC MAKALA ALIPONGEZA

MAFANIKIO YA TRA YAZIDI KUIMARISHA UKUSANYAJI MAPATO ARUSHA

 Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuandika mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato na uboreshaji wa huduma kwa walipakodi, hatua iliyochangia kuimarika kwa ulipaji kodi wa hiari na mazingira salama ya ukusanyaji wa mapato Mkoani Arusha.

Katika kuthibitisha mafanikio hayo, uongozi wa TRA Mkoa wa Arusha leo Jumatatu, Desemba 22, 2025, umemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos  Makalla, katika ofisi yake, kwa lengo la kumshukuru kwa ushirikiano wake wa karibu na mchango mkubwa katika kuhamasisha wananchi na wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kodi kwa hiari.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kuimarisha mahusiano ya kikazi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, yakilenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani humo.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo,  Makalla, akiwa pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Ndugu Misaile Mussa, ameipongeza TRA kwa juhudi zake za kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara na wananchi, akisisitiza kuwa hatua hiyo imeongeza uelewa na imani kwa taasisi hiyo. Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa jukwaa maalum la wadau kutoka sekta mbalimbali ili kukuza majadiliano ya pamoja yatakayosaidia kuongeza mapato ya Serikali kwa uendelevu.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, Deogratius Shuma, amesema TRA itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili walipakodi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali, hatua itakayojenga taswira chanya ya mamlaka hiyo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Makalla ameishukuru TRA kwa kuendelea kuboresha mifumo na huduma za kielektroniki, akibainisha kuwa maboresho hayo yamerahisisha ulipaji kodi kwa wakati, kuongeza uwazi na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa walipakodi.

Ends

Post a Comment

0 Comments