TAZAMA KISHINDO CHA MBUNGE LUKUMAY MWANDETI AKAGUA MRADI MKUBWA WA MAJI AISHINIKIZA SERIKALI KUKAMILISHA MIRADI 9 YENYE THAMANI YA BILIONI 16 ARUMERU MAGHARIBI,SAWA AWA MBOGO KWA WATENDAJI MZIGO

Dkt Lukumay hapoi Aishinikiza Serikali Kukamilisha Miradi 9 ya Maji Arumeru Magharibi

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameiomba Serikali kukamilisha uwekezaji wa miradi tisa (9) ya maji inayotekelezwa katika vijiji mbalimbali vya jimbo hilo yenye thamani ya shilingi bilioni 16.712, ili kuondoa adha ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi.

Dkt. Lukumay alitoa rai hiyo leo desemba 22,2025 wakati wa ziara yake ya kukagua mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 1.026 unaotekelezwa katika Kijiji cha Engalaoni, Kata ya Mwandeti, akisema kukamilika kwa miradi hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa maji yenye madini ya floridi yanayosababisha madhara ya kiafya ikiwemo kuharibika kwa meno na mifupa.

Licha ya mvua kubwa iliyoambatana na baridi kali na ukungu mzito ulioikumba kata hiyo, mbunge huyo alipokewa kwa shamrashamra kubwa kwa mujibu wa mila na desturi za Kimasai, ishara ya heshima, mapenzi na matumaini makubwa waliyonayo wananchi kwake.



 Katika mapokezi hayo ya kimila, mzee mkubwa wa kimila alimfanyia Dkt. Lukumay maombi maalumu ya baraka, akimuombea afya njema, hekima na mafanikio katika uongozi wake. Sambamba na hilo, alizawadiwa shuka maalumu la Kimasai kama ishara ya furaha na shukrani kwa kutembelewa na kiongozi aliyejipambanua kwa vitendo katika kusimamia na kupambania utatuzi wa kero zao.


Akizungumza na wananchi, Dkt. Lukumay aliwashukuru kwa imani waliyoonesha kwake kupitia uchaguzi, huku akiahidi kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Aliisisitiza Serikali kuwalipa wakandarasi wanaodai malipo yao ili waweze kukamilisha miradi iliyopo, hatua itakayopunguza mateso ya wananchi wanaolazimika kutumia maji yasiyo salama.

Aidha, aliwataka madiwani kuorodhesha changamoto zote zilizopo katika kaya zao kwa maandishi na kuziwasilisha katika ofisi yake, ikiwemo changamoto ya nguzo za umeme, ili zipatiwe ufumbuzi kwa ushirikiano.






Kwa upande wao, wananchi walieleza kwa kina changamoto zinazowakabili. Ridhiki Abel, mkazi wa Kitongoji cha Obaa, Kijiji cha Lengijave, alisema changamoto ya maji ni kubwa kiasi kwamba wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 15 kufuata huduma ya maji safi, ambayo nayo hawana uhakika wa kuipata. Alimuomba mbunge kuwachimbia visima au kuwawekea matenki ya maji ili kuwasogezea huduma hiyo muhimu.

Naye Maico Laizer, mkazi wa Kijiji cha Engalaoni, alimkumbusha mbunge juu ya umuhimu wa kutekeleza ahadi, akisema wabunge waliopita wamekuwa na tabia ya kutoa ahadi bila kuzitimiza. Hata hivyo, alimpongeza Dkt. Lukumay kwa uzalendo wake na kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja, akisema utekelezaji wa ahadi utampa uongozi wa muda mrefu.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Engalaoni, Loserian Keya, alimpongeza mbunge kwa ziara hiyo na kueleza kuwa licha ya uwepo wa mradi wa maji, bado changamoto ni kubwa kwani maji ya mradi maarufu kama ‘maji ya vocha’ hutoka mara chache, hivyo kuendelea kuwa kero kwa wananchi.

Diwani wa Kata ya Mwandeti, Longolie Masaandawa, alisema kata hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa za huduma za jamii, akitaja ukosefu wa mtaalamu wa afya katika zahanati ya Kijiji cha Mbibia hali inayosababisha kushindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwandeti. Aidha, alibainisha kuwa miundombinu ya barabara ni kero kubwa na kuomba suala hilo liwekwe kipaumbele.



Katibu wa Siasa na Uenezi (CCM), Nicholus Sawa, alimpongeza Dkt. Lukumay kwa kuwa mbunge wa mfano wa kuigwa kwa kuwafikia wananchi hadi ngazi ya vitongoji bila kuchoka. Aliwakosoa baadhi ya viongozi wa ngazi za chini kwa kushindwa kuwajibika na kusubiri ziara za viongozi wa juu, hali inayochafua taswira ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alitoa wito kwa viongozi hao kuongeza bidii na uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi.

Akigusia changamoto ya mimba za utotoni, Sawa alisema umbali mrefu wa kutembea kwenda shule huwaweka watoto wa kike katika hatari ya unyanyasaji wa kijinsia na ushawishi mbaya, akiwataka wazazi na jamii kwa ujumla kuchukua wajibu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya janga hilo.

Kwa pamoja, baadhi ya wananchi waliomba kujengwa kwa shule nyingine ya sekondari katika eneo hilo ili kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea, jambo litakaloongeza usalama na kuboresha mazingira ya elimu.

Ziara hiyo imeendelea kuonesha dhamira ya kweli ya Dkt. Johannes Lukumay ya kuongoza kwa vitendo, kusikiliza wananchi wake na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akijenga imani na mshikamano mkubwa kati yake na jamii ya Arumeru Magharibi.












Ends..

Post a Comment

0 Comments