LISU ACHAGULIWA MAKAMU MWENYEKITI WA DEMOKRASIA DUNIANI (IDU)

By arushadigtal-ARUSHA


Muungano wa vyama vya kidemokrasia duniani (IDU) umemchagua, Tundu Lissu kuwa mmoja kati ya jopo la makamu wenyeviti wa muungano huo Kanda ya Afrika.


Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema), amechaguliwa sambamba na Waziri Mkuu mstaafu wa 22 wa Canada, Stephen Harper anayeendelea kuwa mwenyekiti wa muungano huo.


Kuchaguliwa kwa Lissu, kumefanyika akiwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi mbili ikiwemo ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni ambapo zinaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.


Taarifa ya kuchaguliwa kwa Lissu, imetolewa leo, Jumamosi Mei 24, 2025 na Chadema ikirejea taarifa ya IDU kuhusu mfululizo wa vikao vyake, vilivyohusisha uchaguzi huo.


Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, uchaguzi wa Lissu na Harper umefanyika jijini Brussels, Ubelgiji vilikokuwa vinafanyika vikao vya muungano huo.


“Katika mkutano huo ambao chama kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Democracy Union of Africa (DUA) Kanda ya Afrika Mashariki, Deogratias Munishi, wajumbe walimchagua Harper kuendelea kuwa mwenyekiti kwa miaka mitatu ijayo,” imeeleza taarifa hiyo.


Sambamba naye, mkutano mkuu huo, kwa kauli moja ulimchagua Lissu kuwa sehemu ya jopo la makamu wenyeviti wa umoja huo.


Ends .

Post a Comment

0 Comments