Na Joseph Ngilisho,ARUSHA
NAIBU waziri Mkuu na waziri wa Nishati,dkt Doto Biteko amewahakikishia wakazi wa Mkoa wa Arusha na Mikoa jirani ya Kilimanjaro na Tanga kupata umeme wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa kuboresha Kituo cha kupoza umeme cha Njiro, kwa kuongeza Transfoma yenye uwezo wa MVA 90,220/132kV,ambapo awali ilikuwa ni MVA120.
Akizungumza na wananchi katika hafla za Sherehe za muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mkoani Arusha, mara baada ya kuzindua kituo hicho Aprili 26, 2025, waziri Biteko alisema kuwa Serikali imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 5.2 kwa ajili ya upanuzi wa Kituo hicho ili kukiongezea uwezo kuendana na ongezeko la matumizi ya umeme.
“Katika ukanda huu, mahitaji ya umeme kwenye Mkoa wa Arusha ni megawati 107, Tanga Megawati 126, Manyara Megawati 14, na Kilimanjaro Megawati 68, na leo tumezindua upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Njiro, ambacho kina njia kumi za kusambaza umeme katika Mkoa wa Arusha na kuuwezesha Mkoa huu kukidhi mahitaji ya umeme kufikia Megawati 200 kulinganisha na mahitaji ya sasa ambayo ni Megawati 107” alisema Dkt. Biteko
Aidha alisema kuwa Serikali ipo kwenye mpango wa utekelezaji wa kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme ikiwa ni maagizo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha miundombinu ya umeme chakavu yote inafanyiwa ukarabati wa njia za kusafirisha umeme.
“Umeme tunaweza kuwa nao kwenye uzalishaji, lakini ikawa changamoto kwenye miundombinu, ndio maana Mhe. Rais ametuagiza sasa kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme ili tuwe na umeme wa uhakika, alisema Dkt. Biteko.
Aliongeza kwa kusema kuwa Wizara ya Nishati imekusudia kuhakikisha kila Mtanzania anapata kipande cha keki ya Nishati hasa Nishati ya umeme.
“Nilipoteuliwa niliwaambia, TANESCO hamtalala usingizi, na wote mnashuhudia kuwa hali ya umeme imebadilika sio kama miaka kumi nyuma, na TANESCO kwa kweli hawalali wanafanya kazi nzuri” alisema Mhe. Dkt. Biteko.
Kukamilika kwa Kituo hicho kutaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Mkoa wa Arusha na kuifungua kiuchumi kwa kukuza Sekta za Utalii, Viwanda na Biashara na hivyo kuchangia Maendeleo makubwa ya Kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya Arusha,Kilimanjaro na Tanga .
Awali taarifa ya Tanesco imesema kuwa kituo cha kupoza umeme cha Njiro ,kilizinduliwa rasmi mwaka 1983 na kimeungwa kwenye gridi ya Taifa kupitia miundombinu ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Singida kupitia wilaya ya Babati na Lemugur .
Taarifa imesema kuwa mradi huo wa uboreshaji wa kituo cha Njiro ambao umekamikika kwa asilimia 100, ulihusisha kukiongezea uwezo kwa kuongeza Transfoma yenye uwezo wa 90MVA ,220/132kV.
"Lengo kuu la utekelezaji wa mradi huu ni kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kupitia Njia za Msongo wa Kilovoti 132 kutoka Megawati 96 za sasa hadi kufikia Megawati 168".
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi wa kampuni ya umeme ya china ya M/S .Xian Electric Engineering co.Ltd kwa fedha za ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 2,272,513.93 sawa na sh,za kitanzania bilioni 5.2.
Mhandisi, Yohana Mtemi.
Naye Mhandisi Yohana Mtemi kutoka kampuni ya Umeme ya Xian Electric Engineering co.ltd inayotekeleza mradi huo kutoka nchini china,alisema mradi wa ufungaji wa Transpoma ya kupooza umeme yenye uwezo wa MVA90 umekamilika na kuwa miongoni mwa Transfoma tatu zenye uwezo mkubwa katika kituo hicho cha Njiro.
Alisema Transfoma hizo zitakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa MVA 210 jambo litakalokuwa chachu ya maendeleo na kuondoa changamoto ya umeme kwa mikoa ya kanda ya kaskazini.
"Mradi huu ulianza Tangu mwaka 2024 na sasa umekamilika kwa asilimia 98 na Transfoma hiyo imeingia kwenye mfumo wa uzalishaji tangu Aprili 14,mwaka huu na mpaka sasa mradi huu upo tayari na wananchi wananufaika"Alisema
Utekelezaji wa Mradi huo ulianza rasmi Mwezi Aprili 2024 na umekamikika kwa asilimia 100 na Transfoma hiyo iliwashwa kwa mafanikio makubwa Aprili 14 mwaka huu 2025 na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa Changamoto ya umeme katika Mkoa wa Arusha na Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Ends...
0 Comments