NGO'S ZAPEWA SOMO NAMNA KUANDAA HESABU ZAO KWA USAHIHI,WATAKIWA KUWATUMIA WAHASIBU KUTOKA NBAA

Na Thobias Mwanakatwe

MASHIRIKA yasiyokuwa ya kiserikali (NGO's) yameshauriwa kuwatumia wahasibu waliosajiriwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) katika kuandaa hesabu zao kwa usahihi ili kujenga hoja za kujitetea kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu kodi wanazozilalamikia.


Mkurugenzi  Mtendaji wa taasisi ya Filadefia inayojishughulisha na utoaji wa mafunzo ya uhasibu, Janjason Kibona,alitoa ushauri huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kufuatia NGO'S kuandaa kitabu chenye malalamiko 25 yaliyoelekezwa kwa TRA kuhusu kodi wanazotozwa.








Alisema NGO's zikiwa zinawatumia wakaguzi wazuri kutoka NBAA wahasibu ambao wana sifa kutakuwa na hesabu nzuri na kuwatetea kwenye suala la kodi kwasababu kutakuwa na ushahidi kwa yule anayekudai.


"Wafadhiri wengi ambao wanatuletea fedha sisi NGO's ni serikali za nchi nyingine,mfano jana tuliona mwakilishi wa Umoja wa Ulaya akieleza wao wanapopewa fedha kuja katika hizi NGO's na wenyewe wanakaguliwa,sasa inapoonekana 'financial statement'haziko sawa maana yake tatizo hilo linaweza kuwa kubwa na kukosa hiyo misaada," alisema Kibona.


Kibona alisema ushauri mwingine kwa NGO's kuepukana na usumbufu ni kuwawezesha wahasibu kushiriki mafunzo maalum yaliyoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kama ambavyo na serikali nayo imekuwa ikifanya ili kuimarisha ufanisi na utendaji kwasababu kanuni za kuandaa hesabu zinabadilika siku hadi siku kulingana na dunia inavyosonga mbele.


"Kama NGO's zitajikita katika kuwa na wahasibu ambao wamebobea katika uandishi wa hizi hesabu wanaweza kuwa na hoja nzuri ambapo hata maandiko yao wanapoomba fedha kwa wafadhiri yatakubaliwa na pia wanapokwenda TRA wanakuwa na pa kuzungumzia," alisema.


Aliongeza kuwa njia nyingine inayoweza kuzisaidia NGO's ni kuwatumia tax consultants ambao wamesajiriwa na TRA wenyewe kama mawakili wa kushughulikia mashauri yao ya kodi kwasababu suala la kodi ni la kisheria.


Kibona alisema kwa kuwa kuna baadhi ya NGO's wajumbe wake ni wabunge kwa hiyo wabunge waanzishe mchakato bungeni wa mabadiliko ya sheria ili zibadilishwe kuzisaidia NGO's zijiendeshe vizuri.


"Huwezi kulalamika kuwa sheria ziondoke hivi hivi mdomoni unatakiwa upeleke hoja bungeni ambapo hoja hiyo ya kubadilisha sheria inaweza kufanyiwa kazi haraka," alisema.


Alisema katika kitabu maalum chenye malalamiko 25 kilichoandikwa na NGO's zinajenga hoja kwamba zinafanya kazi ya kutoa huduma kwa jamii kwa kutumia fedha ambazi ni kodi za serikali nyingine.


Kibona alisema TRA ina kitu kinachoitwa 'service Charter'ambayo inaonesha mkataba wa mlipakodi na TRA ambao ndani yake kuna wajibu TRA katika kutenda kazi za kodi lakini pia kuna wajibu wa NGO's.


"Huu mkataba ndio mzuri ili kuepuka wapi ni wapi na hili likifanyika panaweza kufanyika suluhu ya malalamiko kwani sheria za nchi zipo wazi kwamba NGO's kama taasisi binafsi zinapaswa kuandaa hesabu sahihi kwa kuwatumia wahasibu sahihi," alisema.


Kibona aliongeza kuwa tangu mabadiliko ya sheria yamefanyika 2019 kwa ajili ya kutengeneza mambo mazuri ya kisheria ya kusimamia NGO's vizuri NBAA ilitoa mwongozo kwamba NGO's zote ziweze kuandaa hesabu zao kwa uwazi.


Alisema katika malalamiko ya NGO's nyingi zinagusa suala la elimu, alishauri TRA iwe inatoa elimu kwa taasisi hizo kwa kuwatumia mameneja wa mikoa wa TRA katika mikoa husika ili kuondokana na malalamiko kwamba hazipewi elimu.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments