MAHAKAMA KUU YATENGUA WATOTO WA BILIONEA MREMA WA IMPALA KUSIMAMIA MIRATHI YA BIL 18.3,YATEUA MWINGINE NA KUTOA MIEZI SITA AKUSANYE MALI NA KUGAWA KWA USAWA, WALIOKUWA WASIMAMIZI WAMEZITAFUNA KAMA MCHWA ,

Na Joseph Ngilisho Arusha 

Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha imetengua wasimamizi wa mirathi yenye thamani ya bilioni 18.3 , mali za Marehemu, Melau Mrema aliyefariki mwaka 2017 na kumteua mtoto wa marehemu Randle Mrema kuwa Msimamizi wa mali . 

Randle Mrema

Akisoma hukumu hiyo katika shauri dogo namba 170 la mwaka 2022 lililofunguliwa na Randle Mrema pamoja na Lulu Mrema dhidi ya waliokuwa wasimamizi wa mirathi Janeth Kimaro na Viv Mrema ambao pia ni watoto wa marehemu Mrema.


Jaji Devota Kamzora  alisema kuwa mahakama imezingatia sababu zilizotolewa na waleta maombi ikiwa ni pamoja na waliokuwa wasimamizi wa mali kushindwa kukusanya mali na kulipa madeni pamoja na udanganyifu .


Sababu zingine zilizotolewa na waleta maombi ni wasimamizi hao wa mirathi kujimilikisha mali kwa manufaa yao binafsi pamoja na kutoelewa majukumu yao na kushindwa kugawa mali kwa wanufaika huku wakifanya udanganyifu kwenye nyaraka kuwa wamegawanya wakati wanufaika hawana habari.


Marehemu Mrema alifariki dunia  Julai 30,2017 na kuacha mali mbalimbali ikiwemo nyumba za kupangisha, Mashamba,hoteli,magari , viwanja ,hisa kwenye mabenki,fedha Tasilimu pamoja na miradi ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni nk.

Katika maamuzi ya jaji Kamzora alisema mahakama imegundua kuwa waliokuwa wasimamizi wa mirathi walishindwa kueleza zilipo fedha za  kodi ya majengo zinazolipwa na wapangaji pamoja na hisa za marehemu katika benki ya CRDB katika kipindi cha miaka minne.

Pia mahakama imebaini kuwa kiasi cha sh,bilioni 1.8 kilichokuwa benki hazijulikani zilipo.

Pia waliokuwa wasimamizi wa mirathi walishindwa kuithibitishia mahakama namna walivyogawa mali za marehemu kwa wanufaika na kulipa madeni licha ya wao kuwasilisha nyaraka zinazoonesha kuwa waligawanya mali za marehemu kwa usawa.


Mahakama ilibaini kuwa licha ya wasimamizi kufunga mirathi lakini bado waliendelea kujinufaisha na mali hizo kwa manufaa yao binafsi.


Katika mwenendo wa shauri hilo Mahakama  ilibaini udanganyifu  wa mali halisi za marehemu baada ya kughundua mali zingine zenye thamani ya sh bilioni 15.5 zilikuwa hazijaorodheshwa  .


Katika utetezi wa wajibu maombi kupitia wakili wao George Njooka waliieleza mahakama kuwa walishagawa mali za marehemu kama takwa la sheria linavyosema.


Wakili Njooka alieleza kuwa kumekuwepo na ugumu katika familia hiyo kutokana na mgogoro wa kifamilia uliopo na hivyo kusababisha wasimamizi wa mirathi kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri.


Sababu nyingine  ya kutokamilisha kukusanya na kugawa  mirathi ya marehemu kwa wakati ni pamoja na ukubwa wa madeni na kesi zilizokuwa zikiendelea mahakamani kuhusiana na mali za marehemu. 


Kabla ya maamuzi hayo wakili Njooka aliieleza mahakama athari zinazoweza kujitokeza iwapo mahakama itabatilishwa uamuzi wa wasimamizi wa mirathi ni pamoja na kusababisha gharama kubwa pasipo na msingi 


Katika maamuzi ya jaji Kamzora mahakama imekubaliana na hoja za waleta maombi na hivyo inatengua wasimamizi waliokuwepo na imekubali kumteua Randle Mrema akishirikiana na Lulu Mrema kuwa wasimamizi wa mali za marehemu na kutoa miezi sita kuhakikisha wanakamilisha kukusanya ,kulipa madeni na kugawa mali za marehemu kwa wanufaika .

Hata hivyo mahakama ilisema iwapo kama kuna mali ya marehemu imeuzwa kiuzembe inaweza kufunguliwa mashtaka mahakamani ili kurejesha mali hiyo.


Akiongea nje ya mahakama msimamizi wa mirathi aliyeteuliwa na Mahakama, Randle Mrema ambaye ni mtoto wa marehemu, alisema amepokea uamuzi huo kwa furaha lakini anaona ana deni kubwa la kurekebisha yale yote yaliyotarajiwa kufanywa na wasimamizi waliopita .


Alisema amejipanga kukamilisha   kulipa madeni, kufufua biashara zilizokuwa zimekufa ikiwa ni pamoja na hoteli lakini kushirikiana bega kwa bega na wakurugenzi wengine kwenye makampuni ambayo marehemu alikuwa mmiliki.


Ends..


Post a Comment

0 Comments