Ad
Breaking🔥

MAKALLA AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA KIFO CHA MKENYA NAMANGA

 MAKALLA AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA KIFO CHA MKENYA NAMANGA

...Vurugu za Novemba 4 na 5 zasababisha kuchomwa kwa majengo ya Serikali, kufuatia mwili wa Ian Jackson kukutwa ndani ya kiroba porini na kuzikwa bila kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu

Na Joseph Ngilisho | LONGIDO

MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameunda kamati maalumu ya uchunguzi kubaini mazingira ya kifo cha raia wa Kenya, Ian Jackson, kilichosababisha vurugu za siku mbili, Novemba 4 na 5, 2026, katika eneo la mpakani Namanga, Wilaya ya Longido, zilizoambatana na uchomaji wa baadhi ya majengo ya Serikali upande wa Tanzania.

Vurugu hizo zilitokea baada ya mwili wa Jackson, aliyekuwa akifanya shughuli za forodha katika eneo la Namanga, kukutwa ukiwa umetupwa ndani ya kiroba katika eneo la pori, baada ya kuripotiwa kupotea kwa zaidi ya wiki moja.

Taarifa za awali kutoka kwa watu waliofika au kushuhudia mwili huo zikieleza kuwa kijana huyo alionekana kuwa na majeraha makubwa yanayodaiwa kusababishwa na kukatwa katwa kabla ya mwili wake kuwekwa ndani ya kiroba na kutelekezwa porini.

Hata hivyo, tukio hilo lilizua hasira na maswali miongoni mwa baadhi ya wananchi wa Kenya baada ya Jeshi la Polisi kufika eneo ulikokutwa mwili huo na kuamua kuuzika bila kufanyika kwa uchunguzi wa kitabibu, kwa madai kuwa ulikuwa tayari umeharibika.

Hatua hiyo ilizidisha malalamiko na mvutano, hali iliyochangia kuzuka kwa vurugu zilizoshuhudiwa Novemba 4 na 5, 2026, ambapo baadhi ya raia wa Kenya walifanya uharibifu na kuchoma majengo ya Serikali upande wa Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, Makalla alisema ameunda kamati maalumu ya uchunguzi ili kubaini ukweli wa tukio hilo, mazingira ya kifo cha Jackson na kuwabaini wote waliohusika, akisisitiza kuwa Serikali haitamlinda mtu yeyote atakayethibitika kuhusika na mauaji hayo.

Alisema ameliagiza Jeshi la Polisi kuongoza uchunguzi huo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine husika, huku akihimiza wananchi na vyombo vya usalama vya Kenya kutoa ushirikiano ili ukweli uweze kupatikana.

Makalla alisema Serikali imejipanga kuhakikisha wote watakaobainika kuhusika na mauaji ya kijana huyo wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Alisisitiza kuwa uchunguzi unapaswa kufanyika kwa uwazi na umakini ili kubaini mazingira yote ya tukio hilo, ikiwamo sababu za mwili kuzikwa bila kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na hatua zilizochukuliwa tangu taarifa za kupotea kwa Jackson zilipotolewa.

Katika hatua nyingine, Makalla aliwataka wananchi wa Tanzania na Kenya kuwa watulivu, kuepuka vitendo vya kulipiza kisasi na kulinda amani katika eneo la Namanga, akieleza kuwa vurugu hizo zinaweza kuathiri uhusiano wa kihistoria na ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Alisema Namanga ni eneo muhimu kwa biashara na mwingiliano wa kijamii kati ya Tanzania na Kenya, hivyo ni wajibu wa pande zote kuhakikisha usalama unarejea na shughuli za kiuchumi zinaendelea.

Alisema malalamiko kuhusu kifo cha Jackson yanapaswa kushughulikiwa kwa kufuata sheria badala ya kutumia nguvu, kuchoma majengo au kuharibu mali, vitendo vinavyoweza kuongeza madhara kwa wananchi wa mataifa yote mawili.


Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post