CRDB YAFUNGUA MLANGO WA MABILIONI KWA WACHIMBAJI
....Yasema imewezesha wachimbaji Chunya kwa Sh bilioni 50, yaingia na teknolojia ya CIP kuongeza uzalishaji, yalenga pia madini mkakati
Na Joseph Ngilisho | Dar es Salaam
WAKATI sekta ya madini ikiendelea kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji nchini, Benki ya CRDB imeeleza mkakati wake wa kuongeza nguvu katika ufadhili wa shughuli za uchimbaji, ikiwamo kuwawezesha wachimbaji kupata mitaji mikubwa, teknolojia ya kisasa na huduma maalumu za kifedha ili kuongeza uzalishaji na thamani ya rasilimali zinazozalishwa nchini.
Katika kuonesha namna inavyotekeleza mkakati huo, benki hiyo imetaja uwezeshaji wa kundi la wachimbaji wa Chunya, mkoani Mbeya, kwa mikopo inayofikia Sh bilioni 50, pamoja na kusaidia upatikanaji wa mtambo wa kisasa wa uchakataji dhahabu unaotumia teknolojia ya Carbon-in-Pulp (CIP).
Hatua hiyo inaashiria mwelekeo wa CRDB wa kuunganisha upatikanaji wa mitaji na teknolojia katika shughuli za madini, badala ya kuwawezesha wachimbaji kwa fedha pekee, huku ikilenga kuwasaidia kuondokana na mifumo ya zamani ya uchimbaji na kuingia katika uzalishaji wa kisasa unaozingatia utaalamu.
Akizungumza Nov 20,katika Mkutano wa Wawekezaji wa Madini jijini Dar es Salaam, Meneja Mahusiano wa Kitengo cha Madini wa CRDB Bank, David Minja, alisema benki hiyo imejipanga kuwa mshirika wa kimkakati wa serikali na sekta binafsi katika kufungua fursa za uwekezaji na kuimarisha uwezo wa kifedha wa wadau wa madini.
Alisema CRDB imekuwa ikishirikiana na Tume ya Madini katika kuwawezesha wachimbaji kupata mitaji, kurasimisha shughuli zao na kuboresha mifumo ya uzalishaji ili ziendane na mahitaji ya sekta ya kisasa ya madini.
“Tumekuwa tukishirikiana na Tume ya Madini kuhakikisha tunawawezesha wachimbaji wetu kimitaji, lakini pia kuwasaidia kurasimisha shughuli zao na kufanya uchimbaji kwa kutumia mifumo ya kisasa zaidi,” alisema Minja.
Alisema benki hiyo inaamini kuwa maendeleo ya sekta ya madini yanahitaji uwekezaji katika tafiti, teknolojia na mifumo rasmi ya biashara ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendeshwa kitaalamu na kuwa na uwezo wa kuzalisha kwa tija.
Akizungumzia mfano wa Chunya, alisema uwezeshaji wa wachimbaji wa eneo hilo unalenga kuongeza uwezo wao wa uzalishaji kupitia upatikanaji wa mitaji na teknolojia ya kisasa ya uchakataji.
Alisema mtambo wa CIP utasaidia kuboresha mchakato wa uchakataji wa dhahabu na kuongeza uwezo wa wachimbaji kuendesha shughuli zao kwa kiwango cha kisasa zaidi.
MADINI MKAKATI NAYO KWENYE LENGO
Minja alisema mkakati wa CRDB hauishii katika uchimbaji wa dhahabu pekee, bali unajumuisha madini mengine, gesi asilia na madini ya kimkakati ambayo yanaendelea kufungua fursa mpya za uwekezaji na biashara.
Alisema benki hiyo ina kitengo maalumu kinachojishughulisha na sekta ya madini, kinachofuatilia fursa za uwekezaji na kuandaa huduma zinazowawezesha wateja kushiriki katika miradi mbalimbali inayohusiana na rasilimali za Tanzania.
Alisema uwepo wa kitengo hicho unaifanya benki hiyo kuangalia mahitaji ya kifedha ya sekta kwa mapana yake, ikiwamo kuwawezesha wawekezaji na wadau wanaoshiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na madini.
“Lengo letu siyo biashara ya dhahabu pekee. Tuna madini mengi, gesi asilia na madini mengine ya kimkakati. Tunaangalia fursa zote zinazojitokeza ili kuwawezesha wateja wetu kushiriki na kuwa watekelezaji katika miradi mbalimbali ya rasilimali zilizopo nchini,” alisema.
YALENGA MNYORORO MZIMA WA THAMANI
Katika mkakati wa kupanua huduma zake, Minja alisema CRDB inalenga kwenda zaidi ya utoaji wa mikopo na huduma za kawaida za kibenki kwa kuangalia mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.
Alisema benki hiyo inakusudia kuwafikia wadau wote wanaohusika katika sekta hiyo ili kuhakikisha kila kundi linapata huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya shughuli zake.
Alisema mkakati huo ni muhimu katika kujenga sekta yenye ushindani, kuongeza uwekezaji na kuhakikisha fursa zinazotokana na rasilimali za madini zinawanufaisha wadau wengi zaidi.
Aidha, alisema CRDB inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya uendelevu.
Alisema benki hiyo inaamini kuwa ukuaji wa biashara ya madini haupaswi kutenganishwa na wajibu wa kulinda mazingira na rasilimali kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Ushiriki wa CRDB katika Mkutano wa Wawekezaji wa Madini jijini Dar es Salaam ni sehemu ya ushirikiano wake na Tume ya Madini na wadau wengine wa sekta hiyo katika kuimarisha upatikanaji wa mitaji, kurasimisha shughuli za uchimbaji na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika rasilimali za Tanzania.
Ends

إرسال تعليق