ARUSHA DC YAFIKIA ASILIMIA 80 KUTATUA SAKATA LA MITA 200
Yasema baba wa marehemu Catherine ameanza matibabu, yaandaa ujenzi wa nyumba ya familia hiyo
Yajivunia nafasi ya tano kitaifa Mwenge wa Uhuru, mapato yapanda kutoka Sh bilioni 3.8 hadi 10
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC), Suleiman Msumi, amesema halmashauri hiyo imefikia asilimia 80 ya mafanikio katika kutatua changamoto ya mita 200 Kati ya halmashauri hiyo na Jiji la Arusha,huku akiwatoa hofu madiwani kuwa suala hilo linaelekea kupata ufumbuzi.
Aidha, amesema Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya kuisaidia familia ya marehemu Catherine, mmoja wa wanafunzi watatu wa Shule ya Sekondari Mringa waliofariki katika ajali ya lori lililowadondokea, ikiwamo kuanza matibabu ya baba wa marehemu na maandalizi ya ujenzi wa nyumba ya familia hiyo.
Msumi alitoa kauli hiyo wakati akitoa maelezo ya utekelezaji wa maelekezo na maazimio ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, akisema uongozi na wataalamu wamefanya kazi kubwa kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika suala la mita 200.
Alisema pamoja na kukutana na vikwazo mbalimbali, juhudi zilizofanyika zimewezesha kufikia hatua nzuri na kwamba suala hilo linaendelea kushughulikiwa kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu.
“Kwa sasa tupo katika asilimia 80 ya ushindi katika hili. Madiwani wasiwe na wasiwasi, tulikotoka na hapa tulipofika ni pazuri, ninaamini suala hili linaenda kukaa vizuri kabisa,” alisema Msumi.
AHADI KWA FAMILIA YA CATHERINE
Katika hatua nyingine, Msumi alitoa mrejesho wa ahadi zilizotolewa na Serikali kwa familia ya marehemu Catherine, akisema hatua mbalimbali za utekelezaji zimeanza kufanyika kwa kushirikiana na wadau.
Alisema baba wa marehemu, ambaye alikuwa amelala kitandani kwa takribani miaka miwili bila kupata msaada wa kutosha, tayari amefikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tengeru kwa ajili ya vipimo na matibabu.
Alisema vipimo vimefanyika na matibabu yameanza, huku mpango ukiwa ni kumpeleka katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kukamilika kwa matibabu ya awali.
Kuhusu ujenzi wa nyumba ya familia hiyo, alisema wataalamu wa halmashauri kutoka Idara ya Uhandisi na Ardhi tayari wamefanya upimaji wa eneo na kuchukua viwianishi kwa ajili ya kuanza mchakato wa hati ya umiliki.
Alisema pia mchoro wa nyumba inayotarajiwa kujengwa umekamilika, huku hatua inayofuata ikiwa ni kukamilisha makubaliano ya malipo na mtu aliyeuza eneo hilo ili halmashauri iweze kupata umiliki kamili na kuanza ujenzi.
“Vitu vyote tulivyoahidi kama Serikali vipo kwenye mchakato wa utekelezaji. Mchoro wa nyumba upo tayari, eneo limefanyiwa upimaji na tunachofanya sasa ni kukamilisha suala la umiliki wa eneo,” alisema.
Aliongeza kuwa halmashauri tayari imeanza kutafuta makazi ya muda kwa familia hiyo ili iweze kuhama katika eneo linalotarajiwa kujengwa nyumba, hatua itakayowezesha kufanyika kwa usafishaji na kuanza kwa ujenzi.
ARUSHA DC YASHIKA NAFASI YA TANO KITAIFA
Katika hatua nyingine, Msumi alisema Halmashauri ya Arusha imeibuka nafasi ya tano kitaifa katika matokeo ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, akieleza kuwa mafanikio hayo ni makubwa kutokana na uwezo wa mapato wa halmashauri hiyo.
Alisema halmashauri hiyo imeongeza mapato kutoka Sh bilioni 3.8 ilipokuwa inaanza miaka mitano iliyopita hadi kufikia Sh bilioni 10 inayolenga kukusanya katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Alisema halmashauri hiyo imeongeza mapato kutoka Sh bilioni 3.8 ilipokuwa inaanza miaka mitano iliyopita hadi kufikia Sh bilioni 10 inayolenga kukusanya katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Alisema pamoja na kuwa na uwezo mdogo wa mapato ikilinganishwa na baadhi ya majiji, manispaa na halmashauri nyingine, Arusha DC imeweza kushindana na kupata nafasi hiyo kutokana na ushirikiano wa viongozi na wataalamu.
“Pamoja na udogo wetu, tumeweza kushindana na majiji, manispaa na halmashauri nyingine zenye mapato makubwa na kuibuka nafasi ya tano kitaifa. Hili si jambo dogo, tunastahili kujipongeza,” alisema.
Msumi pia aliwataka madiwani kutumia nafasi zao katika kamati za maendeleo za kata kusaidia kukuza vipaji vya michezo kwa vijana, akisema jukumu hilo halipaswi kuachwa kwa Serikali pekee.
Alimtaja Diwani Mrema kuwa mfano wa kuigwa kutokana na mchango wake katika kusaidia timu na vijana kushiriki mashindano mbalimbali ya michezo, yakiwamo UMISSETA, UMITASHUMTA na SHIMISEMITA.
Aidha, alieleza kuwa halmashauri imepokea maelekezo ya baraza kuhusu changamoto za maji na kwamba imehakikisha Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) anashiriki katika kikao hicho ili kusaidia kutoa ufafanuzi na kutafuta ufumbuzi.
Alisema halmashauri itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na AUWSA kuhakikisha kero za maji zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi zinapatiwa ufumbuzi.
Katika hatua nyingine, aliwataka madiwani na wataalamu kudumisha mshikamano, upendo na kuvumiliana, akisisitiza kuwa tofauti za mawazo hazipaswi kuwa kikwazo katika kutekeleza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi.
Alisema maelekezo na maazimio yote yaliyotolewa katika baraza hilo yamepokelewa na yatafanyiwa kazi, huku akiahidi kutoa mrejesho wa utekelezaji katika vikao vinavyofuata vya kisheria.
Ends



Post a Comment