ZUNGU ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA IPU, ATOA WITO KWA WAFANYABIASHARA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SPIKA wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha, akisema Tanzania iko tayari kuandaa mkutano huo kwa mafanikio.
Zungu alitoa kauli hiyo leo Oktoba 2,2025 jijini Arusha baada ya kukagua maandalizi ya mkutano huo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), huku akiwataka Watanzania, hususan wafanyabiashara, kutumia ujio wa wajumbe kutoka sehemu mbalimbali duniani kujenga fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kitaaluma.Alisema mkutano huo, unaotarajiwa kuwakutanisha mamia ya wajumbe wa kimataifa wakiwamo wabunge, wafanyabiashara, watunga sera na wataalamu, haupaswi kuonekana kama tukio la kibunge pekee, bali ni fursa ya Tanzania kujitangaza na kufungua milango ya masoko na uwekezaji.
“Wengi wanaokuja ni wafanyabiashara na wanasiasa ambao pia wanajihusisha na biashara. Wanahitaji bidhaa mbalimbali na Tanzania ina bidhaa nyingi zenye uwezo mkubwa wa kupata soko,” alisema.
Spika Zungu aliwataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa za Tanzania, akitaja bidhaa za Kimasai, korosho na madini ya Tanzanite kuwa miongoni mwa bidhaa zinazoweza kutafuta masoko kupitia wageni watakaofika nchini.
Alisema Arusha pia inapata fursa ya kujitangaza zaidi kama kitovu cha mikutano ya kimataifa, utalii, biashara na uwekezaji, akiwataka wakazi wa jiji hilo kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kuonyesha ukarimu na kutoa huduma bora kwa wageni.
“Ni fursa kubwa kwa wananchi wa Arusha kushiriki katika shughuli za kimataifa, kiuchumi na kibiashara, kukutana na watu kutoka nchi mbalimbali na kuchangia ukuaji wa Arusha na uchumi wa taifa,” alisema.
Zungu alisema sekta ya utalii na ukarimu inapaswa kutumia ujio wa wageni hao kuimarisha biashara na kuitangaza Arusha kama eneo muhimu la utalii na mikutano ya kimataifa.
Alisema hoteli, migahawa, kampuni za utalii, wasafirishaji, wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali watanufaika na ujio huo, huku huduma bora zikiwa na nafasi ya kuwavutia wageni kurejea Tanzania kwa ajili ya utalii, biashara na uwekezaji.
NCHI 149 ZATHIBITISHA
Akizungumzia maandalizi, Zungu alisema hadi sasa nchi 149 kati ya 183 zinazotarajiwa kushiriki zimeshathibitisha ushiriki wao, huku nchi nyingine zikiendelea kutoa uthibitisho.
Aliwapongeza wahandisi, mafundi, watumishi wa Bunge, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wataalamu wengine wanaoshiriki maandalizi, akisema mchango wao ni muhimu katika kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio.
Pia aliipongeza timu ya IPU iliyopo Geneva pamoja na uongozi wa Bunge kwa kazi wanayoifanya katika kuhakikisha maandalizi yanakamilika kwa wakati.
POSSI: TANZANIA ITAJIONYESHA DUNIANI
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Balozi Dk Abdallah Possi, alisema kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni fursa muhimu ya kujitangaza mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Alisema ni nchi chache barani Afrika ambazo zimewahi kuwa wenyeji wa mkutano wa IPU, hivyo nafasi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania kuonyesha uwezo wake wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa.
“Kwa hiyo Tanzania imepewa fursa muhimu ya kujionesha mbele ya jumuiya ya kimataifa kupitia tukio hili,” alisema Possi.
Alipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, akisema hatua hiyo imeipa nchi nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa.
Possi pia alipongeza Bunge kwa kuchukua jukumu la kuwa mwenyeji mkuu wa mkutano huo na kumshukuru Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na uongozi na watendaji wa wizara hiyo kwa mchango wao katika maandalizi.
Alisisitiza kuwa mkutano huo si tukio la kibunge pekee, bali ni jukwaa la Tanzania kuimarisha diplomasia, kukuza utalii, biashara na uwekezaji pamoja na kujenga uhusiano na mataifa mbalimbali.
Mkutano wa 153 wa IPU unatarajiwa kuwakutanisha wabunge na wadau mbalimbali kutoka sehemu tofauti duniani jijini Arusha.
Ends..





إرسال تعليق