WANAFUNZI 62,079 ARUSHA KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA NNE
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
JUMLA ya wanafunzi 62,079 mkoani Arusha wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 5 na 6, 2026, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Akizungumza ofisini kwake leo, OKTOBA 4,2026 Katibu Tawala Msaidizi, Idara ya Elimu Mkoa wa Arusha, Mwl. Dkt. Vincent Kayombo alisema kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 31,082 sawa na asilimia 50.1, huku wasichana wakiwa 30,997 sawa na asilimia 49.9.
Alisema wanafunzi hao wamesajiliwa kutoka shule 900 za msingi, ambapo shule 587 zinatumia mfumo wa kufundishia kwa Kiswahili na shule 313 zinatumia mfumo wa Kiingereza.
Dkt. Kayombo alisema idadi hiyo ni sehemu ya wanafunzi 83,241 walioandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2023, akibainisha kuwa maandalizi ya mtihani huo yamekamilika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Mitihani ya Taifa.
“Maandalizi yote yameshakamilika kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni za Mitihani ya Taifa. Wasimamizi wote wa mitihani wamepatiwa semina elekezi kuhusu usimamizi wa mitihani hiyo, huku wanafunzi wakiwa wameandaliwa kitaaluma, kiakili na kisaikolojia,” alisema Dkt. Kayombo.
Alisema Serikali inawatakia wanafunzi wote kila la kheri katika mitihani hiyo, huku akiwataka kuwa watulivu, kujiamini na kuzingatia maelekezo wanayopewa na wasimamizi.
Aidha, aliwataka wasimamizi wa mitihani hiyo kuzingatia kikamilifu taratibu na kanuni za Mitihani ya Taifa na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kukiuka taratibu hizo.
Alisema dhamana waliyonayo wasimamizi ni kubwa kwa kuwa inahusisha mustakabali wa wanafunzi wanaowasimamia, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, umakini na weledi.
Awali, Dkt. Kayombo aliwatakia wanafunzi wote mtihani mwema, huku akiwaombea kwa Mwenyezi Mungu wafanye vizuri na kufikia ndoto zao za kielimu na maisha kwa ujumla.
Ends

Post a Comment