VIONGOZI WA DUNIA WATUA ARUSHA KWA IPU
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAGENI na wawakilishi wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani wameendelea kumiminika jijini Arusha, huku maandalizi ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) yakifikia hatua za mwisho kabla ya kuanza kesho kutwa, Oktoba 5, 2026.
Viongozi hao wamewasili jana, Oktoba 3, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Arusha, kwa ajili ya kushiriki mkutano huo mkubwa wa kimataifa unaotarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 2,000 kutoka mataifa mbalimbali wanachama wa IPU.
Wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Bangladesh, Jahrat Adib Chowdhury, aliyewasili akiwa na ujumbe wake, pamoja na Sahiba Gafarova kutoka Bunge la Azerbaijan.
Mkutano huo utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), huku ujio wa viongozi hao ukiendelea kuonyesha nafasi ya Arusha katika kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa inayowakutanisha viongozi na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Kupitia mkutano huo, wabunge wanatarajiwa kupata jukwaa la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu amani, maendeleo, ushirikiano wa kimataifa na ustawi wa jamii, sambamba na kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto na fursa zinazolikabili bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Ujio wa wajumbe hao pia umeongeza mwonekano wa Arusha kama moja ya vituo muhimu vya mikutano ya kimataifa nchini Tanzania, huku sekta mbalimbali za jiji zikitarajiwa kunufaika na uwepo wa maelfu ya washiriki wa mkutano huo.
Mkutano wa 153 wa IPU unafanyika wakati Tanzania ikiendelea kujiandaa kuupokea mkutano huo wa kimataifa, ambao unatarajiwa kuwa miongoni mwa mikutano mikubwa ya mabunge kufanyika nchini.
Ends







Post a Comment