MKANDARASI KUJENGA UWANJA WA NDEGE KWA KASI YA 5G,AANZA KUTEKELEZA MRADI USIKU NA MCHANA,
• Awamu ya kwanza kukamilika Desemba, kukabidhiwa Januari
• Zamu za usiku zaongezwa kuongeza kasi ya ujenzi
• Mradi wa Sh88.5 bilioni kuwezesha ATR 42 kutua
Na Joseph Ngilisho | MANYARA
Mwakilishi wa mkandarasi wa Beijing Construction Engineering Group Company Limited (BCEG), Yuri Cui, alisema utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri na kwamba kwa sasa mkandarasi anaendelea na awamu ya kwanza, inayolenga kukamilisha kazi za msingi za uwanja ikiwemo uwekaji wa tabaka za lami.
“Kwa sasa tuko katika awamu ya kwanza. Mpango wetu ni kukamilisha kazi hii ifikapo Desemba mwaka huu, ikiwemo kuweka tabaka za lami, ili tuweze kukabidhi eneo hili Januari,” alisema.
Alisema baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza, mkandarasi ataingia katika awamu ya pili ambayo, kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa, inatarajiwa kukamilika Juni mwakani.
Akizungumzia ujenzi wa jengo la abiria, Yuri alisema kwa sasa kazi ipo katika hatua ya maandalizi ya msingi, ikiwemo blinding, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa muundo mkuu wa jengo hilo.
Alisema mkandarasi analenga kufikia hatua ya juu zaidi ya ujenzi wa muundo wa jengo hilo ifikapo mwisho wa mwaka huu.
“Kwa jengo la abiria, kwa sasa tunafanya kazi ya blinding. Baada ya hapo tutaendelea na ujenzi wa muundo wa jengo. Tunatarajia ifikapo mwisho wa mwaka tutakuwa tumefikia hatua ya juu ya muundo wa jengo,” alisema.
Alisema kampuni imeongeza muda wa kufanya kazi na kuanzisha zamu za usiku katika eneo la jengo la abiria, huku muda wa kazi ukiongezwa katika maeneo mengine ya mradi.
“Kwa sasa, kwa kuzingatia ratiba tuliyojiwekea, tumeanza pia zamu za usiku katika eneo la jengo la abiria na kuongeza muda wa kazi. Tunatumaini kwa kufanya hivyo tutaweza kukamilisha mradi kwa mujibu wa muda uliopangwa,” alisema.
Kwa upande wake, Project Engineer wa mradi huo, Solomon Dede, alisema ujenzi huo unatekelezwa kwa awamu mbili na umeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya Aerodrome Code 2C.
Alisema mradi unahusisha ujenzi wa runway ya lami yenye urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30, apron kwa ajili ya ndege, pamoja na taxiway yenye urefu wa mita 95 na upana wa mita 65.
Alisema pia mradi unahusisha ujenzi wa jengo la abiria, barabara ya kuingia na kutoka katika eneo la uwanja yenye urefu wa mita 1,274, jengo la ofisi pamoja na majengo ya wahandisi washauri.
“Mradi wetu unaendelea vizuri na tunaujenga kwa awamu mbili. Kwa sasa tuko kwenye awamu ya kwanza na kazi mbalimbali zinaendelea katika eneo la mradi,” alisema.
Dede alisema miongoni mwa kazi zinazoendelea ni ujenzi wa tuta la nje ya runway, jengo la abiria, jengo la ofisi pamoja na maeneo ya wahandisi washauri.
Alisema hadi sasa mkandarasi amelipwa Sh14.75 bilioni, zikiwamo fedha za malipo ya awali na malipo kwa kazi zilizotekelezwa.
Dede alisema malipo hayo yamewezesha mkandarasi kuendelea na utekelezaji wa mradi bila kukwama, huku akisema Serikali imeendelea kuhakikisha fedha zinapatikana na malipo yanafanyika.
“Tunashukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kufanya malipo kwa wakandarasi kwa wakati na hivyo kazi zinaendelea vizuri,” alisema.
Dede alisema mhandisi mshauri anayesimamia mradi amemwelekeza mkandarasi kuongeza vifaa, nguvu kazi na muda wa kufanya kazi ili kuongeza kasi ya utekelezaji.
Alisema hatua hiyo inahusisha kufanya kazi usiku na mchana katika maeneo yanayohitaji kasi zaidi, lengo likiwa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.
“Tumemwelekeza mkandarasi kuongeza vifaa vya kufanya kazi, kuongeza nguvu kazi na muda wa kufanya kazi, ikiwamo kufanya kazi usiku na mchana, ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyotakiwa,” alisema.
Dede alisema baada ya kukamilika, uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege aina ya ATR 42, huku ukiwa na miundombinu na vifaa vya usalama vitakavyowezesha shughuli za ndege kufanyika mchana na usiku.
“Baada ya kukamilika kwa mradi huu, uwanja utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege aina ya ATR 42. Kwa kuwa utakuwa na vifaa vyote vya usalama, kutakuwa na shughuli za ndege zinazofanyika muda wote, usiku na mchana,” alisema.
Alisema uwanja huo unalenga kuimarisha usafiri wa anga na kuongeza fursa za kiuchumi na utalii katika Mkoa wa Manyara, huku usimamizi wa mradi ukiendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa mkandarasi.
Mradi huo ulianza Desemba 18, 2020, huku mkataba wa awali ukiainisha kukamilika Juni 18, 2024. Kwa sasa, utekelezaji unaendelea kwa ratiba iliyoboreshwa huku hatua zikichukuliwa kuongeza kasi ya kazi.
Ends










Post a Comment