VIJIJI 60% HAVINA MIPANGO YA ARDHI
...Mmuya ataka TEHAMA kudhibiti migogoro; Lugangira, Kalimenze na Mkupasi waibua changamoto za usimamizi na upungufu wa wataalamu
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imeweka lengo la kuhakikisha vijiji vyote nchini vinakuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ifikapo mwaka 2030, huku takwimu zikionyesha kuwa ni asilimia 40 pekee ya vijiji vilivyofikiwa na mipango hiyo, hali inayochangia changamoto za usimamizi wa ardhi na migogoro ya matumizi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, alisema kukamilisha mipango hiyo na kusimamia utekelezaji wake ni muhimu katika kudhibiti mwingiliano wa matumizi ya ardhi, kulinda maeneo yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali na kuharakisha maendeleo endelevu.Mmuya alitoa kauli hiyo Oktoba 28,2026 jijini Arusha alipomwakilisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Wataalamu wa Mipango Miji.
Alisema wataalamu wanapaswa kuimarisha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kupanga, kusimamia na kufuatilia matumizi ya ardhi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na kupunguza migogoro inayotokana na ukiukwaji wa mipaka.
Alisema mifumo ya kidijitali itawawezesha wataalamu kupata taarifa za maeneo kupitia kompyuta na simu, badala ya kutegemea ramani za karatasi ambazo wakati mwingine hufanya utambuzi wa maeneo kuwa mgumu.Alisisitiza kuwa wataalamu hawapaswi kuishia kuandaa mipango, bali wanapaswa kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa makazi, kilimo, uwekezaji na huduma za kijamii yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema ofisi moja ya mipango miji inahudumia zaidi ya watu 100,000, hali inayoongeza mzigo kwa wataalamu waliopo wakati mahitaji ya makazi, miundombinu na huduma za kijamii yakiendelea kuongezeka.
Kalimenze alisema matumizi ya teknolojia kama TEHAMA, akili unde (AI), mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS) na picha za anga yanaweza kuongeza ufanisi katika kupanga, kusimamia na kufuatilia maendeleo ya miji.
Aidha, aliwapa wataalamu wa mipango miji miezi mitatu kukamilisha taratibu za usajili katika bodi husika, akisisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma lazima uzingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Alisema marekebisho ya sheria ya mwaka 2023 yalipanua makundi yanayotakiwa kusajiliwa, hivyo akawataka wataalamu ambao hawajakamilisha taratibu hizo kutumia muda waliopatiwa kufanya hivyo.
LUGANGIRA AONYA VIONGOZI
Lugangira, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CP Amos Makalla, alisema ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali na wataalamu ni muhimu katika kulinda mpangilio wa makazi, mazingira na rasilimali zinazochangia uchumi wa mkoa huo, hususan utalii.
Alisema Arusha inahitaji mipango inayozingatia mabadiliko ya wakati na mahitaji ya wananchi ili kuhakikisha ukuaji wa miji na vijiji hauathiri matumizi yaliyopangwa kisheria.
Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji (TPRB), TP. Martha Mkupasi, alisema bodi hiyo imesajili wataalamu 818 na kampuni 119 tangu kuanzishwa kwake.Alisema katika mwaka wa fedha 2025/26, bodi ilisajili wataalamu 191, wakiwamo 27 wenye usajili kamili na 164 wa ngazi ya wahitimu, huku pia ikifuta usajili wa wataalamu 36 na kampuni 15 kutokana na ukiukwaji wa maadili ya taaluma.
Mkupasi alitaja ufinyu wa bajeti, ukosefu wa fedha za mafunzo na utekelezaji wa kazi za mipango miji na watu wasio na sifa zinazotakiwa kisheria kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Aliiomba Serikali kuharakisha uteuzi wa bodi mpya baada ya iliyokuwepo kumaliza muda wake Novemba 2025, akisema kuchelewa kwa uteuzi kunaweza kuathiri maamuzi yanayohitaji kufanywa na bodi na kamati zake.
TITP YATAKIWA KULINDA TAALUMA
Rais wa Chama cha Wataalamu wa Mipango Miji Tanzania (TITP), Dkt. Juma Matindana, alisema chama hicho kinapaswa kuzingatia misingi ya kitaaluma na kuepuka kugeuzwa kuwa chama cha harakati.
Alisema jukumu lake ni kukuza weledi, kutetea maslahi ya taaluma na kutafuta suluhisho la changamoto za upangaji na udhibiti wa maendeleo ya miji.
Matindana alisema sekta binafsi na taasisi za elimu zinapaswa kushirikishwa zaidi katika kupanga na kuendeleza miji, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kutumia utaalamu uliopo na kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji.
Mkutano huo wa 11 unajadili namna mabadiliko ya kidijitali yanavyoweza kuboresha taaluma ya mipango miji, kudhibiti ukuaji wa miji na kuimarisha matumizi endelevu ya ardhi nchini.
Ends








Post a Comment