SERIKALI YARIDHISHWA KASI YA MIRADI YA BARABARA ARUSHA
........YATAKA TAASISI ZOTE KUSHIRIKIANA KUKAMILISHA KABLA YA AFCON
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi ya barabara jijini Arusha kuelekea mashindano ya AFCON, huku ikizitaka wizara, mashirika na taasisi mbalimbali kushirikiana kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, alisema maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya AFCON ni jukumu la Serikali nzima, hivyo taasisi zote zinazohusika zinapaswa kushirikiana katika kutatua changamoto na kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi.
Kadogosa alisema hayo Oktoba 6,2026 jijini Arusha wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya barabara inayotekelezwa katika jiji hilo, akisema ziara hiyo imemuwezesha kuona hali halisi ya utekelezaji na changamoto zinazohitaji hatua za Serikali.
“Nimekagua barabara hizi zote, nimefurahishwa sana na kasi ya ujenzi wa barabara hizo. TANROADS wanafanya kazi nzuri sana na kwa kasi hii wanayoendelea nayo inaonyesha miradi hiyo itamalizika kwa wakati na kwa muda uliopangwa,” alisema.
Alisema Serikali haitaki kuona miradi hiyo ikichukuliwa kuwa ya muda mfupi kwa sababu ya AFCON, bali inapaswa kutazamwa kama uwekezaji wa muda mrefu wenye manufaa kwa wananchi na uchumi wa Arusha.
“Barabara hizo hazijengwi kwa ajili ya AFCON pekee, bali ni uwekezaji wa muda mrefu utakaosaidia kuifungua Arusha, kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo utalii na biashara,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, alisema barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa ina urefu wa takribani kilomita 70 kutoka Mbauda hadi Losinyai, mpakani mwa Arusha na Manyara, huku kilomita 13 zikiwa sehemu ya kipaumbele katika maandalizi ya AFCON.
Alisema kilomita 7.4 kutoka Mbauda hadi makutano na Arusha Bypass zinajengwa kwa njia nne pamoja na barabara za huduma kila upande, huku taa zikiwekwa katika eneo lote linalopita mjini.
Massawe alisema kipande kingine cha kilomita 5.6 kinachoungana na Arusha Bypass kinajengwa kwa njia mbili kutokana na kiwango cha magari kinachotarajiwa kutumia barabara hiyo.
Alisema ujenzi wa kilomita hizo 13 unafanywa na kampuni ya CCECC ya China kwa gharama ya takribani Sh221 bilioni, huku Serikali ikiwa imelipa takribani Sh21 bilioni kama malipo ya awali na utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 50.93.
Alisema TANROADS inaendelea kumsimamia mkandarasi kuongeza rasilimali, mitambo na nguvu kazi ili kuhakikisha vipande hivyo vinakamilika ndani ya muda uliopangwa kabla ya mashindano ya AFCON.
Aidha, Massawe alisema kuna mradi mwingine unaoanzia Arusha mjini katika eneo la Chuo cha Ufundi, kupitia Kona ya Nairobi kuelekea Uwanja wa Ndege wa Arusha na Kisongo, pamoja na maeneo mengine yanayounganisha mtandao wa barabara wenye urefu wa takribani kilomita 40.
Alisema mradi huo unajengwa kwa njia nne pamoja na njia mbili za huduma na unatekelezwa na kampuni ya China kwa gharama ya takribani Sh77 bilioni, huku malipo ya awali ya takribani Sh12 bilioni yakiwa yamefanyika.
Massawe alisema TANROADS pia imepewa jukumu la kujenga mtaro wa maji wenye urefu wa kilomita moja katika eneo la Sambasha kutokana na changamoto ya maji na mmomonyoko katika maeneo ya milimani.
Alisema utekelezaji wa mtaro huo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika muda mfupi, huku Serikali ikiendelea kushirikisha taasisi mbalimbali katika kutatua changamoto za maji, fidia na masuala mengine yanayoweza kuchelewesha miradi.
Alisema kwa ujumla, mradi wa kilomita 18 unaotekelezwa katika maeneo hayo una thamani ya takribani Sh22 bilioni, huku Serikali ikiendelea kuhakikisha miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa manufaa ya muda mrefu kwa wananchi wa Arusha.
Ends

Post a Comment