Ad
Breaking🔥

NAESA KUWAJENGEA UWEZO MAAFISA UGANI MIKOA 14 KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

 NAESA KUWAJENGEA UWEZO MAAFISA UGANI MIKOA 14 KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

Na Hadija Bagasha Tanga, 

Wakulima katika mikoa 14 nchini wanatarajiwa kunufaika na huduma bora za ugani kufuatia mpango wa Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA) wa kuwajengea uwezo maafisa ugani kutafsiri taarifa za hali ya hewa na kuzifikisha kwa wakulima kwa wakati, hatua inayolenga kuboresha maamuzi ya kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji.


Mafunzo hayo yanatarajiwa kutolewa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, yakilenga kuwawezesha maafisa ugani kutumia taarifa za hali ya hewa kuwashauri wakulima kuhusu maandalizi ya mashamba, muda sahihi wa kupanda na mbinu zinazofaa kulingana na mazingira ya maeneo yao.


Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya kilimo ikiendelea kuhitaji taarifa sahihi na huduma za kitaalamu zitakazowawezesha wakulima kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kupunguza changamoto zinazoweza kuathiri uzalishaji wa chakula.


Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Usagara, jijini Tanga, Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji Thamani wa NAESA, Ester Mwaisango, alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza ufanisi wa maafisa ugani katika kuwafikishia wakulima taarifa muhimu kwa wakati.


Alisema maafisa ugani wana nafasi kubwa katika kuhakikisha wakulima wanapata maarifa yanayowawezesha kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kilimo, hivyo ni muhimu kuwajengea uwezo wa kuchambua na kutumia taarifa zinazohusu mwenendo wa hali ya hewa.


Mwaisango alieleza kuwa mafunzo hayo yatahusu maeneo yenye misimu miwili ya mvua, yakiwemo Kanda ya Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mikoa ya Morogoro na Kigoma.


Alisema ushirikiano kati ya NAESA na Wizara ya Kilimo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za ugani kwa kuhakikisha maarifa yanayopatikana yanawafikia wakulima na kutumika kuboresha shughuli zao za uzalishaji.


WAKULIMA MILIONI 5.5 WASAJILIWA


Katika hatua nyingine, Mwaisango alisema NAESA inaendelea kusimamia na kuratibu shughuli za maafisa ugani nchini, zikiwemo usajili wa wakulima katika mifumo rasmi, ambapo zaidi ya wakulima milioni 5.5 wamekwishasajiliwa.


Alisema zoezi la usajili linaendelea, likiwa sehemu ya juhudi za kuboresha uratibu wa huduma za kilimo na kuongeza ufanisi katika kuwafikia wakulima kwa huduma zinazohitajika.


Kwa mujibu wa Mwaisango, majukumu mengine ya wakala huo ni kuratibu huduma za ugani wa kilimo nchini, kusimamia vyuo vya mafunzo ya kilimo na vituo vya mafunzo kwa wakulima, pamoja na kuratibu huduma zinazohusiana na zana za kilimo.


Aliongeza kuwa NAESA pia inahamasisha kilimo biashara, inaandaa miongozo ya ufundishaji na kushirikiana na vyuo vya kilimo kuboresha mitaala inayotumika katika kuwafundisha maafisa ugani.


Alisema juhudi hizo zinalenga kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya wakulima na mabadiliko yanayotokea katika sekta ya kilimo.


TEKNOLOJIA YA MVUKE KUONGEZA THAMANI YA MPUNGA


Mbali na mafunzo kwa maafisa ugani, NAESA ilitumia maadhimisho hayo kuonesha teknolojia mbalimbali zinazofundishwa katika vyuo vya kilimo, zikiwemo mbinu za uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke kabla ya kukobolewa.


Teknolojia hiyo inalenga kuboresha ubora wa mchele na kupunguza kiwango cha mchele kinachovunjika wakati wa ukoboleaji, hivyo kutoa fursa kwa wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na kunufaika zaidi na shughuli za kilimo.


Akizungumzia teknolojia hiyo, Hamisi Ramadhani kutoka Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Ulenga kilicho chini ya NAESA alisema wameona umuhimu wa kuwafundisha wakulima mbinu zinazoweza kuongeza tija na mapato yao.


Alisema wakulima wengi wamekuwa wakiuza mpunga wakiwa bado shambani au kupeleka mazao yao kwenye mashine za kawaida za kukoboa, hali inayoweza kuwanyima fursa ya kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza.


Ramadhani alisema matumizi ya mvuke katika uchakataji wa mpunga yanaweza kusaidia kuboresha ubora wa mchele na kupunguza kiasi cha mchele kinachovunjika wakati wa kukobolewa.


Aliongeza kuwa kuwafundisha wakulima teknolojia hizo ni sehemu ya juhudi za kuwapa maarifa yatakayowawezesha kuchakata mazao yao kwa ubora zaidi, kupanua fursa za masoko na kuongeza kipato.


Alisema msisitizo wa kutumia maarifa na ubunifu katika kilimo ni muhimu katika kuwasaidia wakulima kuboresha uzalishaji na kupata manufaa zaidi kutokana na mazao wanayozalisha.


Ushiriki wa NAESA katika maadhimisho hayo uliambatana na wawakilishi kutoka vyuo vinavyotoa mafunzo ya uhamishaji wa teknolojia za kilimo, ambao walieleza mbinu mbalimbali zinazoweza kutumiwa kuboresha uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.

Post a Comment

أحدث أقدم