Ad
Breaking🔥

MOTO WATEKETEZA VYUMBA 10 PANGANI ARUSHA, WAKAZI WAPOTEZA MALI ZOTE MWINGINE APOTEZA LAKI TANO ZA MAREJESHO ALIACHA MEZANI

MOTO WATEKETEZA VYUMBA 10, WAKAZI WAPOTEZA MALI ZOTE ARUSHA

Na Joseph Ngilisho| ARUSHA 

MOTO mkubwa umeteketeza vyumba 10 vya nyumba ya makazi iliyopo Mtaa wa Pangani, Kata ya Kati, Wilaya ya Arusha Mjini, na kusababisha wakazi kupoteza mali zao zote, zikiwamo fedha taslimu Sh500,000.

Nyumba hiyo iliyokuwa na zaidi ya vyumba 14 ilikumbwa na moto huo usiku, huku juhudi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zikifanikiwa kuudhibiti kabla haujasambaa katika ghorofa ya pili ya jengo hilo.

Akizungumza eneo la tukio, OKTOBA 30,2026 Kamanda wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Oswald Mwanjejele, alisema walipokea taarifa ya tukio hilo saa 4 usiku na askari walipofika walikuta moto ukiwa umesambaa kwa kiwango kikubwa.

Alisema pamoja na kufanikiwa kuuzima moto huo, chanzo chake bado hakijajulikana, ingawa uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa mitungi ya gesi iliyopasuka ndani ya nyumba hiyo.

“Bado hatuna uhakika kwamba chanzo ni gesi, lakini mitungi ya gesi tuliyoikuta ikiwa imepasuka inaweza kuwa sehemu ya chanzo. Uchunguzi utaendelea kubaini chanzo halisi,” alisema.

Mwanjejele alitaja changamoto mbili zilizokwamisha juhudi za kuudhibiti moto huo kwa wakati kuwa ni kuchelewa kupatikana kwa taarifa pamoja na kuzibwa kwa njia zilizokuwa zikitumiwa na magari ya zimamoto kufika eneo la tukio.

Alisema kutokana na hali hiyo, askari walilazimika kuvuta mabomba ya maji kwa umbali wa takribani mita 100 kupitia mitoni ili kufika eneo lililokuwa likiungua.

“Changamoto nyingine ni kwamba njia zilizokuwa zikiruhusu magari ya zimamoto kupita zimezibwa, hivyo ilitubidi kuzungusha mabomba kwa umbali mrefu ili kufikisha maji eneo la tukio,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa wakazi wa nyumba hiyo, Christina Mas, alisema wakati moto unatokea hakuwa nyumbani na aliporejea baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani alikuta nyumba ikiwa imeteketea.

Alisema anaishi na familia ya watu saba na hakufanikiwa kuokoa mali yoyote, akieleza kuwa aliondoka nyumbani akiwa amewaacha watoto wake na kurejea kukuta kila kitu kimeungua.

Kwa upande wake, mkazi mwingine wa eneo hilo alisema taarifa alizozipata kutoka kwa jirani zinaeleza kuwa moto huenda ulianza baada ya gesi iliyokuwa ikitumika kupikia kuvuja na kuwaka.

Alidai kuwa baada ya gesi hiyo kuwaka, kulikuwa na jaribio la kumwaga maji ili kuuzima, lakini moto uliendelea kusambaa. Hata hivyo, maelezo hayo bado hayajathibitishwa na uchunguzi wa mamlaka husika.

Mkazi huyo alisema katika mali zilizoteketea ni pamoja na fedha taslimu Sh500,000 alizokuwa ameziacha mezani kwa ajili ya kurejesha deni la mtu siku iliyofuata.

Hadi sasa hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa au kupoteza maisha katika tukio hilo, lakini familia zilizoathirika zimepoteza makazi na mali zao zilizokuwa ndani ya vyumba vilivyoungua.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post