Ad
Breaking🔥

GWAJIMA ATOA ONYO KWA WATUMISHI, AITAKA WIZARA ILETE MATOKEO KWA WANANCHI

GWAJIMA ATOA ONYO KWA WATUMISHI, AITAKA WIZARA ILETE MATOKEO KWA WANANCHI

...Asema utekelezaji wa Dira 2050 hautapimwa kwa matumizi ya fedha pekee, ataka taarifa za bajeti kuwasilishwa kabla ya mwisho wa Oktoba

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameitaka menejimenti na watumishi wa wizara hiyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuimarisha uwajibikaji, nidhamu na ufanisi ili kuhakikisha kila rasilimali inayotumika inaleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayawezi kupimwa kwa kiasi cha fedha kilichotengwa au kutumika pekee, bali kwa namna huduma zinavyowafikia wananchi, changamoto zinazotatuliwa na matokeo yanayopatikana katika jamii.

Dkt. Gwajima alitoa msisitizo huo leo Oktoba 15, 2026, jijini Arusha, alipofungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa PAPU International Conference Center (PICC), akielekeza watumishi kuhakikisha mipango, bajeti na programu za wizara zinakuwa na matokeo yanayopimika.

Alisema wizara hiyo ina jukumu muhimu katika kujenga mtaji watu na kuimarisha ustawi wa jamii, hivyo utekelezaji wa majukumu yake unapaswa kuendana na matarajio ya wananchi pamoja na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alieleza kuwa huduma za malezi na ulinzi wa mtoto, ustawi wa familia, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, huduma kwa wazee na makundi maalum ni maeneo yanayohitaji ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha walengwa wanapata huduma bora na fursa za kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

“Huduma za maendeleo na ustawi wa jamii ni uwekezaji katika mtaji watu na uwezo wa Taifa. Ni lazima kuhakikisha programu tunazotekeleza zinakuwa na manufaa halisi kwa wananchi na zinachangia kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.

Aitaka menejimenti kuwajibika

Katika hatua nyingine, Dkt. Gwajima aliitaka menejimenti kuimarisha usimamizi wa watumishi, kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wafanyakazi zinashughulikiwa kwa haki na kwa wakati.

Alisema utendaji wenye tija unahitaji ushirikiano kati ya menejimenti na watumishi, mashauriano katika kutatua changamoto na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Aliwataka watumishi kuzingatia weledi, uadilifu na nidhamu ya kazi, huku wakitumia teknolojia kuboresha utendaji na kuimarisha uratibu kati ya idara na vitengo vya wizara.

Alisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kuelewa wajibu wake katika kufanikisha malengo ya taasisi, akieleza kuwa uwajibikaji unapaswa kuonekana katika kazi zinazofanyika na huduma zinazotolewa, badala ya kuishia kwenye mipango na taarifa za utekelezaji.

Bajeti kupimwa kwa matokeo

Akizungumzia utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri huyo alisema tathmini ya robo ya kwanza inapaswa kuangalia kwa pamoja fedha zilizopokelewa, matumizi yaliyofanyika, shughuli zilizotekelezwa na matokeo yaliyopatikana kwa wananchi.

Alielekeza taarifa za utekelezaji wa bajeti kuwasilishwa kabla ya mwisho wa Oktoba mwaka huu, huku menejimenti ikitakiwa kufanya ufuatiliaji wa maendeleo kila mwezi ili kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua za kuzitatua.

Alisema usimamizi wa karibu wa rasilimali za umma ni muhimu katika kuhakikisha fedha zinatumika kwa madhumuni yaliyoidhinishwa na kuleta thamani inayotarajiwa.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya mipango ya wizara, matumizi ya fedha za umma na matokeo yanayotarajiwa katika utoaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Naibu  Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, alisema mafanikio ya wizara yanategemea uwajibikaji, nidhamu ya kazi na ushirikiano wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao.

Alisema watumishi wanapaswa kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazozikabili jamii na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinawafikia walengwa kwa wakati.

Mahundi alieleza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji jamii yenye uwezo wa kutatua changamoto zake, kutumia fursa zilizopo na kushiriki katika kuleta maendeleo endelevu.

Alisisitiza umuhimu wa watumishi kutambua nafasi yao katika kufanikisha azma hiyo kupitia utendaji wenye tija na utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Mwenyekiti wa kikao hicho, Wakili Amon Mpanju, alisema wizara imejikita katika kuboresha maslahi ya watumishi, mazingira ya kazi na upatikanaji wa vitendea kazi vinavyohitajika katika kutekeleza majukumu yao.

Alisema hatua hizo zinalenga kuwawezesha watumishi kufanya kazi kwa ufanisi, kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mpanju alieleza kuwa mazingira bora ya kazi na upatikanaji wa vitendea kazi ni sehemu muhimu ya kujenga utendaji wenye tija, huku ushirikiano kati ya menejimenti na wafanyakazi ukiwa nguzo ya kufikia malengo ya wizara.

Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi unafanyika wakati wizara ikisisitiza umuhimu wa kuoanisha utendaji wake na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali, uwajibikaji wa watumishi na ubora wa huduma za maendeleo ya jamii.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم