ZARA YAZINDUA ‘TWENZETU KILELENI’ MSIMU WA TANO
.....Watalii zaidi ya 200 kulenga kilele cha Kilimanjaro kusherehekea miaka 65 ya Uhuru
Na Joseph Ngilisho | Dar es Salaam
KAMPUNI ya Zara Tanzania Adventures imezindua rasmi msimu wa tano wa kampeni ya “Twenzetu Kileleni 2026”, inayolenga kuhamasisha Watanzania kushiriki katika kupanda Mlima Kilimanjaro na kusherehekea miaka 65 ya Uhuru wa Tanganyika.Kampeni hiyo iliyozinduliwa jana, Septemba 10, 2026 katika Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dar es Salaam, inatarajiwa kuwashirikisha zaidi ya watalii 200 watakaopanda Mlima Kilimanjaro kupitia Njia ya Marangu, wakilenga kufika kileleni wakati wa maadhimisho ya Uhuru Desemba 9.
Alisema Zara imeweka gharama nafuu ya Sh1.8 milioni kwa mtu, ambayo inajumuisha huduma mbalimbali ikiwamo malazi, chakula, vifaa, usafiri na tozo za Serikali.
“Lengo letu ni kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa ya kutembelea na kupanda Mlima Kilimanjaro, huku tukitumia kampeni hii kuendelea kuitangaza Tanzania na vivutio vyake,” alisema Mama Zara.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro itafanyika kuanzia Desemba 5 hadi 10, 2026, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 65 ya Uhuru.
TWENZETU SERENGETI
Mbali na kampeni ya Twenzetu Kileleni, Zara Tanzania Adventures imezindua pia kampeni ya “Twenzetu Serengeti”, inayolenga kuwawezesha Watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika msimu mzima wa Desemba.
Safari hiyo itaanzia Springlands Hotel, Moshi, kwa gharama ya Sh1.2 milioni kwa mtu, kwa safari ya siku nne.
Zara imesema kifurushi hicho kitajumuisha usafiri kwa magari ya Land Cruiser 4x4, chakula, vinywaji baridi, malazi pamoja na ada za kuingia hifadhini, huku kila gari likibeba watu saba.
TISEZA YAUNGA MKONO
Kwa upande wake, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji kutoka TISEZA, Daudi Liganda, alisema taasisi hiyo inaunga mkono juhudi za Zara Tanzania Adventures katika kukuza na kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini.
Liganda alisema TISEZA pia itashiriki katika kampeni hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro, akieleza kuwa si mara ya kwanza kwa taasisi hiyo kushiriki zoezi hilo.
“Sisi TISEZA mwaka huu tutaungana na Zara kupanda kileleni. Si mara yetu ya kwanza, tumewahi kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka 2021. Tunataka kuiambia dunia kwamba Tanzania ni mahali salama kwa uwekezaji na kuhamasisha watu waje kuwekeza,” alisema.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii na uwekezaji, wakiwamo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), TTCL, TISEZA, BUMACO, MSD na Chuo cha Taifa cha Utalii, pamoja na wadau wengine.
Ends..



Post a Comment