Breaking🔥

TARURA YAONGEZA KASI BARABARA ZA AFCON KABLA YA EL NINO

TARURA YAONGEZA KASI BARABARA ZA AFCON KABLA YA EL NINO

Na Joseph Ngilisho | Arusha

BODI ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeagiza kuharakishwa kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali ya Uwanja wa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) jijini Arusha, kabla ya kuanza kwa mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba, 2026.



Agizo hilo limetolewa baada ya Bodi hiyo kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo, ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 60, huku ikisisitiza kuwa kazi zinazoweza kukamilishwa kabla ya mvua zipewe kipaumbele.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA, Mhandisi Florian Kabaka, amesema ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, lakini amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kukamilisha kazi zinazoweza kufanyika kabla ya mvua kuanza.

Amesema ziara hiyo imelenga kukagua maendeleo ya miradi, utekelezaji wa mikataba pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wahusika ili kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

“Tumetembelea miradi yote na kwa ujumla inaendelea vizuri. Nia yetu kubwa ni kujionea wenyewe maendeleo ya kazi na kusisitiza kwamba iendane na muda uliopangwa. Hatutaki kuona changamoto zinazoweza kuzuilika zikijitokeza baadaye,” amesema Mhandisi Kabaka.

Amesema kutokana na utabiri wa mvua za El Nino, mkandarasi anatakiwa kupanga kazi zake kwa kuzingatia hali ya hewa ili kuepusha uharibifu wa miundombinu na kuchelewesha utekelezaji wa mradi.

Mhandisi Kabaka amesema kazi zinazoweza kufanyika bila kutegemea maji mengi, ikiwemo baadhi ya kazi za udongo na ujenzi wa madaraja, zinapaswa kupewa kipaumbele na kukamilishwa kabla ya mvua kuanza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, amesema ziara hiyo imehusisha ukaguzi wa barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali ya Uwanja wa AFCON, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Mei, 2027.

Amesema TARURA inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa mujibu wa mikataba, muda uliopangwa na viwango vinavyotakiwa.

Mhandisi Seff amemtaka Mhandisi Mshauri wa mradi huo, M/s Afrisa Consulting LTD, kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa kazi, hasa zile zinazoweza kukamilishwa kabla ya msimu wa mvua, ili kupunguza uwezekano wa uharibifu wa miundombinu.

Aidha, amemtaka mkandarasi M/s China Railway Construction Engineering Group kufanya tathmini upya ya utayari wa mradi kukabiliana na mvua za El Nino na kuwasilisha taarifa ya hatua zilizochukuliwa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kuhakikisha mvua zinazotarajiwa kuanza Oktoba, 2026 hazisababishi madhara makubwa wala kuathiri kasi ya utekelezaji wa mradi unaolenga kukamilika kabla ya AFCON.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم