SH. BILIONI 35 KUMALIZA KERO YA MAJI MKINGA.
Na Hadija Bagasha Tanga,
Serikali imeanza kutekeleza mradi wa Sh bilioni 35 wa kusambaza maji katika Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga, hatua inayotarajiwa kumaliza changamoto ya muda mrefu ya uhaba wa maji kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Kauli hiyo imetolewa jana, Septemba 25, na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, wakati akizungumza na wananchi wa Mkinga katika ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga.
Kihongosi alisema utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Mkinga, akieleza kuwa kukamilika kwake kutabadilisha hali ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Alisema Serikali imeendelea kuelekeza fedha katika miradi ya maendeleo ikiwamo maji, afya, elimu na miundombinu, kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi.
“Mradi huu wa maji utakapokamilika, changamoto ya uhaba wa maji kwa wakazi wa Wilaya ya Mkinga itakuwa historia,” alisema Kihongosi.
Kwa mujibu wa risala iliyosomwa wakati wa uzinduzi wa shina hilo, uhaba wa maji ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkinga.
Hivyo, mradi huo wa Sh bilioni 35 unaibua matarajio mapya kwa wakazi wa wilaya hiyo, ambao kwa muda wamekuwa wakikabiliwa na changamoto katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa maisha ya kila siku na shughuli za kiuchumi.
Kihongosi alisema uwekezaji huo wa maji ni sehemu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Tanga, akitaja pia miradi mikubwa ya kimkakati iliyotekelezwa katika mkoa huo.
Alitaja Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima, Uganda, hadi Chongoleani, Tanga, pamoja na upanuzi wa Bandari ya Tanga, kuwa miongoni mwa miradi mikubwa yenye umuhimu katika uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
“Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi ambayo imeacha alama kubwa Mkoa wa Tanga kama Bomba la Mafuta, upanuzi wa Bandari ya Tanga na miradi mingine mikubwa,” alisema.
Katika ziara hiyo, Kihongosi pia alikagua ujenzi wa nyumba 36 za watumishi wa CCM katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Tanga, mradi unaolenga kuboresha mazingira ya kazi na makazi kwa watendaji wa chama.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Rajabu Abrahman, alisema ujenzi wa nyumba hizo unalenga kuwapatia watumishi makazi bora ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa utulivu.
“Serikali ya CCM inaposema inaleta maendeleo kila mahali inamaanisha, kama mnavyoshuhudia umeme, barabara na miradi ya maji,” alisema Abrahman.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Mfaume Kizigo, alisema tathmini ya kihandisi inaonyesha kuwa ujenzi wa nyumba hizo 36 unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 2.5 hadi kukamilika.
Alisema tayari Sh bilioni moja zimetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurahman, kwa ajili ya kuendeleza utekelezaji wa mradi huo.
Kizigo alisema awali Abdurahman alitoa Sh milioni 54, huku Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) wa Mkoa wa Tanga akitoa Sh milioni 10 kwa ajili ya mradi huo.
Pamoja na masuala ya maendeleo, Kihongosi aliwataka wananchi wa Mkinga kuendelea kulinda amani, upendo na mshikamano uliopo katika jamii.
Aliwataka wananchi kuwa makini na kauli zinazoweza kuibua chuki na migawanyiko miongoni mwao, akisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja katika kipindi hiki.
“Mvikatae vyama vinavyoeneza maneno ya chuki na kuwatenganisha. CCM ni chama kinachowajali na kuwaletea maendeleo,” alisema.
Kwa hatua hiyo, utekelezaji wa mradi wa Sh bilioni 35 wa maji unaweka matarajio mapya kwa wananchi wa Mkinga, huku Serikali ikieleza kuwa kukamilika kwake kutasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji na kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wakazi wa wilaya hiyo.
MWISHO





Post a Comment