CCM ARUMERU YAWATAKA VIONGOZI KUTOKA OFISINI KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI
Na Joseph Ngilisho | ARUMERU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arumeru kimewataka madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutoka maofisini na kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua changamoto zao, kikisema baadhi ya kero zinaweza kutatuliwa papo hapo bila kusubiri hatua kutoka ngazi za juu.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Noel Severe, katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lembulung Lukumay, uliofanyika katika Kata ya Nduruma, wilayani Arumeru.Severe alisema ziara za viongozi za kuwafikia wananchi na kusikiliza kero zao zinapaswa kuwa utaratibu wa kawaida, akiwataka madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuhakikisha wanakwenda kwenye maeneo ya wananchi badala ya kusubiri wananchi wafike ofisini.
“Wananchi hawa ni watu wema sana na wanakipenda Chama Cha Mapinduzi, lakini lazima viongozi mtoke mkawasikilize. Kuna kero nyingine ni ndogo, mkikaa tu mnatakiwa mzimalize papo hapo,” alisema.Alisema amefurahishwa na namna Dkt Lukumay anavyotekeleza wajibu wake wa kuwawakilisha wananchi, akisema mbunge huyo amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali ya jimbo, kusikiliza kero na kuzifikisha katika mamlaka husika kwa ajili ya hatua.
Severe alisema viongozi wengine wanapaswa kuiga utaratibu huo kwa kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kueleza changamoto zao moja kwa moja kwa viongozi wanaowahudumia.
AMWAGA SIFA KWA LUKUMAY
Severe alimpongeza Dkt Lukumay kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, akisema nafasi hiyo ni muhimu na inapaswa kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wa Arumeru na Taifa kwa ujumla.
“Tumepata bahati kubwa sana ya mbunge wetu kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge. Lazima tutembee vifua mbele kwa kujivunia,” alisema.
Alisema nafasi hiyo inampa Dkt Lukumay jukumu kubwa katika kusimamia masuala yanayohusu sekta ya afya, huku akiwataka wananchi na viongozi wa eneo hilo kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.
ASEMA ‘TUACHE KUPIGANA SHOTO’
Katika hatua nyingine, Severe aliwataka viongozi wa chama na Serikali kuacha migogoro na misuguano isiyokuwa na tija, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa umoja, mshikamano na amani.
“Tuache kupigana shoto, tufanye kazi kwa umoja, mshikamano na amani. Amani yetu lazima tuilinde kwa nguvu zote,” alisema.
Alisema amani ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za kijamii, akiwataka wananchi na viongozi kuilinda na kuenzi.
DARaja LA NDURUMA
Severe pia alizungumzia suala la ujenzi wa daraja linalohitajika na wananchi wa Nduruma, akisema tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa baada ya changamoto hiyo kufikishwa kwa viongozi.
Alisema wataalamu walishafika eneo hilo kwa ajili ya kufanya tathmini, uchunguzi na usanifu, huku hatua za maandalizi ya bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo zikiwa zimeanza.
“Hili suala la daraja kwa wananchi wa Nduruma ni muhimu sana. Litawasaidia bodaboda, akina mama na wananchi wengine ambao wamekuwa wakipata changamoto katika eneo hili,” alisema.
Alisema CCM Wilaya ya Arumeru itaendelea kushirikiana na Dkt Lukumay kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi, akisisitiza kuwa chama kiko tayari kusukuma utekelezaji wa mradi huo kwa manufaa ya wananchi.
AIPA MBEGU ZA USHIRIKIANO
Severe aliwataka wananchi, viongozi wa CCM, Serikali za mitaa na wataalamu kuendelea kufanya kazi kwa mshikamano katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Alisema viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi na kuhakikisha kero zinazoweza kutatuliwa katika ngazi za chini zinapatiwa ufumbuzi bila kucheleweshwa.
Ends



Post a Comment