Ad
Breaking🔥

SERIKALI KUTENGA SH BILIONI 10 KUANZA MAANDALIZI YA MELI MPYA YA MIZIGO

SERIKALI KUTENGA SH BILIONI 10 KUANZA MAANDALIZI YA MELI MPYA YA MIZIGO

Na Hadija Bagasha|TANGA

SERIKALI imetenga Sh bilioni 10 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa meli mpya ya mizigo, inayolenga kuimarisha usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na nchi jirani kupitia Bahari ya Hindi.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa usafirishaji wa majini, kurahisisha biashara, kuchochea uwekezaji na kuongeza fursa za ajira zinazohusiana na sekta ya usafiri wa majini.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, alitoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani yatakayofanyika mkoani humo kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2026.

Alisema Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) imekamilisha utafiti wa mahitaji ya soko katika mwambao wa Bahari ya Hindi, hatua iliyosaidia kubaini aina na mahitaji ya meli inayofaa kujengwa kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo.

“Serikali imetenga Sh bilioni 10 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa meli mpya ya mizigo,” alisema.

Alisema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha sekta ya usafiri majini kwa kuboresha miundombinu ya bandari, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria, kuimarisha usalama wa vyombo vya majini na kuongeza uwezo wa utafutaji na uokoaji.

Kwa mujibu wa Balozi Burian, ujenzi wa meli hiyo utasaidia kuongeza nafasi ya usafiri wa majini katika kurahisisha biashara na usafirishaji wa bidhaa, huku ukifungua fursa kwa sekta mbalimbali zinazohusiana na uchukuzi wa majini.

BANDARI YA TANGA

Akizungumzia maendeleo ya sekta hiyo mkoani Tanga, Balozi Burian alisema Serikali imeendelea kuboresha Bandari ya Tanga, hatua ambayo imeongeza ufanisi wa huduma na kuchochea ongezeko la shughuli za usafirishaji wa mizigo pamoja na meli zinazofika katika eneo hilo.

Alisema uwekezaji huo umeifanya sekta ya usafiri majini kuwa kichocheo muhimu cha shughuli za kiuchumi mkoani Tanga, ikiwamo biashara, uwekezaji, utalii na ajira.

Alisema Serikali pia imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo, sambamba na kuongeza usalama wa vyombo na abiria wanaotumia usafiri wa majini.

Aidha, alisema Serikali imeendelea kutoa nafasi zaidi kwa sekta binafsi kushiriki katika uendeshaji na uendelezaji wa shughuli za bandari na huduma za usafiri majini, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuvutia uwekezaji.

SIKU YA USAFIRI MAJINI

Balozi Burian alisema Tanga imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Usafiri Majini Duniani mwaka huu, akizishukuru taasisi mbalimbali zilizohusika katika maandalizi.

Alisema maadhimisho hayo ya siku nne yatajumuisha shughuli mbalimbali za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu usalama wa usafiri majini, wajibu wa mabaharia na mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi.

Alisema pia kutakuwa na maonyesho ya huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali na wadau wa sekta ya usafiri majini, pamoja na kampeni za kuhamasisha wananchi kutumia vyombo vya majini kwa kuzingatia taratibu za usalama.

Alisema kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Septemba 24, 2026, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Alisema shughuli za awali zinatarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Khalid Mohamed.

Balozi Burian alisema maadhimisho hayo yanaipa Tanga fursa ya kuonyesha nafasi yake katika sekta ya usafiri majini kutokana na uwepo wa Bandari ya Tanga na mwambao mpana wa Bahari ya Hindi.

Post a Comment

Previous Post Next Post