Breaking🔥

MTANZANIA APEWA DHAMANA KUONGOZA KAMPUNI YA PAN-AFRIKA YA UFADHILI WA MASHINE

MTANZANIA APEWA DHAMANA KUONGOZA KAMPUNI YA PAN-AFRIKA YA UFADHILI WA MASHINE

NaMWANDISHI WETU|ArushaDigita|

MTANZANIA, Nicomed Bohay, amepewa dhamana ya kuongoza kampuni ya Pan-Afrika ya EFAfrica Group Ltd, baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu (Group CEO), hatua inayoongeza nafasi ya wataalamu wa Tanzania katika uongozi wa taasisi za kimataifa za kifedha.

Bohay, ambaye ana uzoefu wa karibu miaka 30 katika sekta ya fedha za maendeleo, benki, biashara za kilimo na ujasiriamali, atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za EFAfrica katika Tanzania, Kenya, Zambia na Mauritius.

Katika nafasi hiyo, atahakikisha utekelezaji wa mkakati wa kampuni wa kupanua huduma za ufadhili wa mashine na vifaa vya uzalishaji, kwa lengo la kuwawezesha wakulima, wafanyabiashara, viwanda, kampuni za ujenzi na usafirishaji kupata mitambo na mashine za kisasa bila kulazimika kuwa na mtaji mkubwa wa awali.

Akizungumzia uteuzi huo, Mwenyekiti Mtendaji wa EFAfrica Group, Dk. Michiel Timmerman, alisema Bohay amekuwa akionyesha uwezo mkubwa wa uongozi, nidhamu katika usimamizi na dhamira ya kuimarisha ujumuishi wa kifedha kupitia ufadhili wa vifaa vya uzalishaji.

“Nicomed ameonyesha uongozi wa kipekee, nidhamu katika usimamizi na dhamira ya kweli ya kuimarisha ujumuishi wa kifedha kupitia ufadhili wa vifaa vya uzalishaji. Tuna imani kuwa ataiongoza EFAfrica kufikia hatua mpya ya ukuaji na athari kubwa zaidi kwa wakulima na biashara za Afrika,” alisema Dk. Timmerman.

Kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo, Bohay alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Equity for Tanzania Limited (EFTA), kampuni inayojihusisha na ufadhili wa mashine na vifaa vya uzalishaji kupitia mfumo wa leasing.

Alijiunga na EFAfrica mwaka 2021, baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust Tanzania na pia kuongoza Idara ya Biashara za Kilimo katika Benki ya CRDB.

Katika kipindi cha uongozi wake EFTA, kampuni hiyo ilipanua kwa kiwango kikubwa huduma zake za ufadhili wa mashine, huku ikiimarisha nafasi yake katika kusaidia sekta ya kilimo, usafirishaji, ujenzi, viwanda na biashara ndogo na za kati.

Taarifa za fedha za mwaka ulioishia Juni 2026 zilionyesha kuwa kiwango cha mikopo chechefu kilikuwa asilimia moja pekee, jambo linaloelezwa kuwa ni kiashiria cha usimamizi mzuri wa biashara na nidhamu katika utoaji wa huduma za kifedha.

Chini ya uongozi wa Bohay, zaidi ya mashine 4,000 za kilimo zimefadhiliwa kwa wakulima, zikiwemo matrekta, power tillers, combine harvesters na mifumo ya umwagiliaji.

Ufadhili huo umewezesha wakulima kuongeza uwezo wa uzalishaji, kupunguza utegemezi wa zana duni za kilimo na kuchangia katika kuimarisha uzalishaji wa chakula.

Mbali na kilimo, EFTA imewezesha maelfu ya biashara kupata malori, mabasi, mashine za viwandani, vifaa vya ujenzi na mitambo ya uchakataji kupitia mfumo wa leasing.

Hatua hiyo imeongeza uwezo wa uzalishaji kwa wafanyabiashara na kampuni mbalimbali, huku ikichangia upanuzi wa biashara na uundaji wa ajira.

Katika eneo la ujumuishi wa kiuchumi, Bohay pia alisimamia kuanzishwa kwa Mpango wa Ukodishaji wa Vifaranga na Chakula cha Kuku unaolenga wanawake na vijana.

Kupitia mpango huo, wanufaika hupata vifaranga, chakula na pembejeo muhimu kwa mfumo wa leasing, hatua inayowawezesha kuanzisha au kukuza shughuli za ufugaji bila kuhitaji mtaji mkubwa wa kuanzia.

Akizungumzia dira yake katika nafasi mpya, Bohay alisema anataka kuhakikisha ukosefu wa mashine na vifaa vya uzalishaji hauwi kikwazo kwa wakulima na wafanyabiashara wa Afrika kufikia ukuaji wa kiuchumi.

“Tunataka EFAfrica iwe mshirika wa kwanza wa wakulima na wafanyabiashara katika safari yao ya ukuaji. Tukiwapa watu vifaa vya kuzalisha, tunawapa uwezo wa kubadilisha maisha yao na kuchochea uchumi wa Afrika,” alisema.

Uteuzi wa Bohay unatajwa kuwa ni hatua nyingine inayodhihirisha kuongezeka kwa nafasi ya wataalamu wa Kitanzania katika kuongoza taasisi zinazofanya kazi katika masoko mbalimbali ya Afrika.

Katika nafasi yake mpya, anatarajiwa kutumia uzoefu alioupata katika sekta ya fedha, kilimo na ufadhili wa vifaa vya uzalishaji kuendeleza huduma za EFAfrica na kuongeza upatikanaji wa mitaji ya uzalishaji kwa wafanyabiashara na wakulima barani Afrika.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم