KWAGILWA AAGIZA KIKAO CHA SIKU TATU KUTATUA TATIZO LA MAJI A TO Z
Na Joseph Ngilisho | Arusha
Kwagilwa alitoa agizo hilo leo September 14,2026 baada ya kutembelea kiwanda hicho na kubaini uwepo wa changamoto katika mfumo wa mifereji na uelekezaji wa maji ya mvua, hali aliyosema inaweza kusababisha maji kuelekezwa kwenye makazi ya wananchi wakati wa mvua kubwa.
Alisema ni muhimu suala hilo kutatuliwa mapema kwa kuwa kutokamilika kwa mifumo ya mifereji kunaweza kusababisha mafuriko, kuathiri wananchi wanaozunguka eneo hilo na hata kuathiri shughuli za uzalishaji kiwandani.
“Haya maji lazima yatafutwe pa kwenda. Huwezi ukaacha culvert hii kubwa halafu imuage maji mahali ambako haieleweki yanaenda wapi. Mapema sana hapa patatuletea shida kwa wananchi. Hata kiwanda hiki kitashindwa kufanya kazi,” alisema.
Kwagilwa alisema uwekezaji unaofanywa na A to Z, ikiwamo shughuli za uzalishaji, ajira na ulipaji wa kodi, ni muhimu kwa uchumi, hivyo Serikali haiwezi kusubiri hadi changamoto za mazingira zigeuke kuwa tatizo kubwa kwa wananchi na kiwanda.
Aliagiza kikao hicho chini ya uongozi wa Mkoa wa Arusha kihusishe TARURA, TANROADS, mamlaka ya maji pamoja na Jiji la Arusha, ili kila taasisi iweze kutoa mchango wake katika kupata suluhisho la kudumu.
“Kikao kikae ndani ya siku tatu na ndani ya siku saba nataka kupata taarifa ya nini mpango uliopo mahali hapa,” alisema.
Alimtaka Mkuu wa Wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo hilo kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa, huku taarifa ya hatua zilizochukuliwa ikiwasilishwa ndani ya siku saba.
Aidha, Naibu Waziri alitaka uchunguzi ufanyike kuhusu mradi wa mfereji unaodaiwa kuwa na thamani ya Sh2.5 bilioni, akitaka kufahamishwa kiasi cha fedha kilichotolewa na Serikali, matumizi yake na sababu za mradi huo kutokamilika.
Alisema katika baadhi ya maeneo bado kuna mashimo na sehemu ambazo mifereji haijaunganishwa ipasavyo hadi eneo lililokusudiwa kupokea maji, hali inayoweza kuongeza hatari ya mafuriko.
A TO Z YAIONYA TANROADS
Wakati huo huo, Meneja wa Afya, Usalama na Mazingira wa A to Z, Mhandisi Harryson Rwehumbiza, alisema kampuni hiyo imebaini changamoto katika mfumo wa maji ya mvua kwenye baadhi ya barabara zinazojengwa na TANROADS, akionya kuwa maji yanaweza kuelekezwa kwenye makazi ya wananchi.
Alisema ujenzi wa barabara unapaswa kwenda sambamba na uwekaji wa mfumo madhubuti wa drainage ili maji yasitoke kwenye barabara na kuingia kwenye maeneo ya makazi.
“Tumegundua barabara inayotengenezwa na TANROADS haijawekewa mfumo halisi wa kupeleka maji ya mvua yanapokwenda. Maji yanayotokana na barabara yanaelekezwa kwenye makazi ya watu, lakini hawajaweka mfumo halisi wa kuboresha drainage system,” alisema.
Rwehumbiza alisema A to Z imepokea kwa uzito maelekezo ya Naibu Waziri, akieleza kuwa kampuni hiyo tayari imewekeza katika mfumo wa kutibu majitaka kabla ya kuyaachia kwenye mazingira.
Alisema kampuni pia inashirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) katika ujenzi wa bomba la majitaka litakalounganishwa kwenye mfumo mkuu wa majitaka wa jiji, lakini kazi hiyo imechukua karibu miaka mitatu bila kukamilika.
“Maelekezo ya Waziri tumeyapokea vizuri sana kwa sababu kiwanda kina mfumo halisi wa kupeleka majitaka. AUWSA wanajenga bomba la sewage kupeleka kwenye mfumo mkuu wa jiji, lakini kazi hiyo imechukua karibu miaka mitatu na mpaka sasa bomba hilo halijaunganishwa,” alisema.
A TO Z YAREJESHA MATUMIZI YA MAJI
Rwehumbiza alisema A to Z imeendelea kutumia teknolojia ya kutibu na kurejesha matumizi ya maji, hatua inayolenga kupunguza matumizi makubwa ya maji na uchafuzi wa mazingira.
Alisema maji yanayotokana na majitaka baada ya kutibiwa hutumika tena katika shughuli mbalimbali, ikiwamo kumwagilia bustani na baadhi ya shughuli za uzalishaji.
“Tunavyotreat haya majitaka, tunayaondoa uchafu na yanakuwa maji ya kawaida. Haya maji tunayafanya recycle, tunamwagilia gardens, bustani na pia tunatumia tena kwenye production upande wa boiler,” alisema.
Alisema kampuni inaendelea kushirikiana na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha shughuli zake zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za mazingira.
Rwehumbiza alisema pongezi zilizotolewa na Naibu Waziri baada ya kukagua mifumo ya usimamizi wa mazingira kiwandani zimeongeza ari kwa kampuni kuendelea kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira.
Ends..














إرسال تعليق