Ad
Breaking🔥

DC KALI ATAKA UNYWAJI WA MAZIWA UWE UTAMADUNI WA NYUMBANI NA MASHULENI

MAZIWA YAINGIA KIPAUMBELE LISHE YA WATOTO

......awataka wazazi, walimu, wanafunzi kuyanywa kila siku; Msalya asema Tanzania ina uwezo wa kujitosheleza

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUU wa Wilaya ya Longido, Salumu Kali, amewataka wazazi, walimu na wanafunzi nchini kujenga utamaduni wa kunywa maziwa nyumbani na shuleni kila siku, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha lishe, afya na ukuaji wa watoto.

Kali alisema maziwa hayapaswi kuonekana kuwa sehemu ya maadhimisho ya siku maalumu pekee, bali yawe sehemu ya mlo wa kila siku wa watoto na familia, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuwekeza katika uzalishaji wa maziwa kupitia ufugaji wa kisasa.

Alitoa kauli hiyo Septemba 29, 2026, jijini Arusha, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Unywaji wa Maziwa Shuleni Duniani, yaliyoandaliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB).

“Maziwa si kwa ajili ya maadhimisho ya leo pekee. Tujenge utamaduni wa kunywa maziwa kila siku, nyumbani na shuleni, kwa sababu mtoto mwenye lishe bora ana nafasi nzuri ya kukua, kujifunza na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” alisema Kali.

Alisema uwekezaji katika lishe ya watoto ni uwekezaji wa moja kwa moja katika nguvu kazi ya taifa, kwa kuwa watoto wenye afya bora wana uwezo mkubwa wa kujifunza na baadaye kushiriki katika uzalishaji na ujenzi wa uchumi.

“Mtoto tunamjengea lishe bora leo, ndiye atakayekuwa daktari, mwalimu, mwanasayansi, mwanasheria, kiongozi au mzalishaji wa taifa kesho. Kwa hiyo kila hatua tunayochukua leo kuboresha lishe ni uwekezaji katika taifa la kesho,” alisema.

Kali alisema Serikali inaendelea kuimarisha mpango wa unywaji wa maziwa shuleni, akibainisha kuwa mafanikio ya mpango huo yanahitaji ushirikiano kati ya TDB, wazazi, walimu, sekta ya mifugo, sekta binafsi, wafugaji, wasindikaji na wadau wengine.

Alisema ongezeko la matumizi ya maziwa linaweza pia kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kuongeza soko la bidhaa hiyo na kuwapa fursa wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na wawekezaji katika viwanda.

“Maziwa si suala la lishe pekee, pia ni fursa ya uchumi. Tukiongeza matumizi ya maziwa, tunaongeza mahitaji, tunamfungulia mfugaji soko, tunaongeza uzalishaji na tunachochea mnyororo mzima wa thamani,” alisema.

Aliwataka wafugaji kuongeza uzalishaji wa maziwa bora na salama kwa kutumia mbinu za kisasa za ufugaji, lishe bora ya mifugo, huduma za afya ya mifugo pamoja na kuzingatia usafi wakati wa kukamua na kuhifadhi maziwa.

Pia aliitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi, usafirishaji na usambazaji wa maziwa ili kuongeza thamani na kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia walaji ikiwa salama na yenye ubora.

TANZANIA YALENGA KUJITOSHELEZA

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Profesa George Msalya, alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kujitosheleza kwa maziwa kutokana na wingi wa mifugo na rasilimali zilizopo nchini.

Profesa Msalya alisema elimu inayotolewa kwa watoto kuhusu umuhimu wa maziwa ni sehemu ya maandalizi ya kizazi kitakachokuja kuwa nguvu kazi na wadau wa sekta hiyo.

“Tunawashukuru sana kwa kutoa elimu kwa watoto hawa ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa la Tanzania. Tunawaona hapa wadau wa tasnia ya maziwa, wajasiriamali, wamiliki wa viwanda na wafugaji ambao ni sehemu ya utajiri wa taifa letu,” alisema.

Alisema Tanzania ina takribani ng’ombe milioni 40, huku ng’ombe wa maziwa wakifikia takribani milioni 1.4, akisema idadi hiyo ni fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji na kukuza sekta ya maziwa.

Kwa mujibu wa Profesa Msalya, Tanzania huzalisha takribani lita bilioni 4.2 za maziwa kwa mwaka, lakini kiwango hicho bado hakitoshelezi mahitaji ya taifa, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji na kuimarisha mnyororo mzima wa thamani.

“Tunayo maziwa mengi, lakini bado hayatoshi. Kwa hiyo utaona kwamba taifa limepiga hatua kubwa, lakini tunahitaji kuongeza uzalishaji zaidi,” alisema.

Profesa Msalya alisema Tanzania yenye ardhi, mifugo na rasilimali nyingine haipaswi kutegemea chakula kutoka nje, akisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa ndani ili kukidhi mahitaji ya wananchi yanayoongezeka sambamba na ongezeko la watu.

“Hatupaswi kuwa taifa la kuomba chakula. Tunahitaji kuwa taifa linalojitosheleza kwa chakula kwa sababu tuna utajiri mkubwa wa mali, mifugo na watu,” alisema.

WITO KWA WANAFUNZI

Kwa upande wake, Kali aliwataka wanafunzi kuanza kujenga utamaduni wa kuchagua vyakula vyenye virutubisho, akiwataka kutumia kwa busara fedha wanazopewa na wazazi au walezi kwa ajili ya matumizi ya shule.

“Afya yako ndiyo mtaji wako wa kufanya vizuri katika masomo na maisha. Ukipewa fedha za matumizi, tumia sehemu yake kununua vyakula vinavyojenga mwili, ikiwamo maziwa,” alisema.

Alisema kaulimbiu ya maadhimisho hayo inayosisitiza “Nyumbani, Shuleni, Maziwa kwa Lishe Bora” inapaswa kutafsiriwa kwa vitendo kwa kuhakikisha watoto wanapata maziwa nyumbani na kuendelea kuyapata wanapokuwa shuleni.

Alisema sekta ya maziwa pia ina nafasi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia kuimarisha usalama wa chakula na lishe, kuongeza ajira na kipato cha kaya, kukuza viwanda na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Maadhimisho hayo ya kitaifa yaliyofanyika mkoani Arusha yalihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa, yakilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa, hususan kwa watoto wa shule, pamoja na kukuza mnyororo wa thamani wa sekta hiyo kuanzia kwa mfugaji hadi kwa mlaji.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم