Ad
Breaking🔥

BALOZI MATINYI ATEMBELEA KIWANDA CHA MASHINE ZA KUSINDIKA MAZAO ALGERIA

BALOZI MATINYI ATEMBELEA KIWANDA CHA MASHINE ZA KUSINDIKA MAZAO ALGERIA

Na Mwandishi Wetu | ALGIERS

BALOZI wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, amefanya ziara katika kiwanda cha kampuni ya CAM SARL, nje kidogo ya Jiji la Algiers, kujadili uwezekano wa kampuni hiyo kushirikiana na Tanzania katika utengenezaji wa mashine za kusindika na kufungasha mazao ya kilimo.

Ziara hiyo iliyofanyika jana, Septemba 23, 2026, imelenga kuangalia fursa za teknolojia na uwekezaji katika kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini Tanzania kabla ya kuuzwa katika masoko ya ndani na kimataifa.

Katika ziara hiyo, Balozi Matinyi alifanya mazungumzo na timu ya menejimenti ya CAM SARL iliyoongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Bouzid Belhadj, akishirikiana na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Abderraouf Belhadj, pamoja na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Alaaeddine Belhadj.

Mazungumzo hayo yalijikita katika uwezekano wa kampuni hiyo kutengeneza mashine zitakazokidhi mahitaji mahsusi ya Tanzania katika uchakataji, usindikaji na ufungashaji wa mazao ya kilimo.

Balozi Matinyi alisema Serikali ya Tanzania imeweka sera na mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo nchini ili kuwawezesha wakulima na wazalishaji kupata masoko yenye tija zaidi, ikiwamo masoko ya kimataifa.

Alisema Tanzania ina fursa kubwa katika sekta ya kilimo kutokana na uzalishaji wa mazao mbalimbali, yakiwamo matunda, mbogamboga, viungo, nafaka, korosho, karanga, alizeti, chai na kahawa.

Kwa mujibu wa Balozi Matinyi, upatikanaji wa teknolojia sahihi za uchakataji na ufungashaji unaweza kusaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Alisema ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Algeria unaweza kuwa msingi wa kampuni za Algeria kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za Tanzania katika kuleta teknolojia, utaalamu na uwekezaji unaohitajika katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CAM SARL, Bouzid Belhadj, alimshukuru Balozi Matinyi kwa kutembelea kampuni hiyo na kueleza utayari wa kuendeleza mawasiliano na Tanzania.

Belhadj pia aliahidi kufanya ziara nchini Tanzania ili kujionea kwa karibu fursa zilizopo, mahitaji ya soko na maeneo ambayo kampuni hiyo inaweza kushirikiana na wadau wa Tanzania.

CAM SARL ni kampuni inayotengeneza mashine za kusindika na kufungasha bidhaa za kilimo pamoja na bidhaa za dawa za tiba, huku ikitumia wataalamu wa Algeria na teknolojia kutoka Ujerumani, Italia na Hispania.

Kampuni hiyo tayari imeanza kupanua soko lake katika nchi jirani na Algeria, ikiwamo Tunisia, hatua inayoiweka katika nafasi ya kushirikiana na masoko mengine ya Afrika.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم