ARUSHA YATAKA SHULE ZOTE KUINGIA KWENYE MPANGO WA MAZIWA
..Katibu Tawala asema ni msingi wa lishe na afya ya kizazi kijacho
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, amewataka wadau wa sekta ya maziwa kuongeza kasi ya kuingiza shule nyingi zaidi katika mpango wa ununuzi na unywaji wa maziwa shuleni, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha lishe na afya ya watoto nchini.
Dkt. Nguvila ametoa wito huo leo Septemba 29,2026 jijini Arusha wakati wa Kongamano la Wadau wa Maziwa kuelekea maadhimisho ya Siku ya kilele cha Unywaji wa Maziwa Shuleni Septemba 30,2026...Katika jiji la yatafanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ngarenaro yakiwa na ujumbe uliobeba kaulimbiu “Nyumbani, Shuleni Maziwa Lishe Bora.”
Amesema mpango wa unywaji wa maziwa shuleni unapaswa kupewa kipaumbele na wadau wote kwa kuwa unalenga kuwajengea watoto utamaduni wa kutumia maziwa tangu wakiwa wadogo, huku wakipata virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji na maendeleo yao.
Kwa mujibu wa Dkt. Nguvila, ongezeko la shule zinazotekeleza mpango huo litasaidia kuwafikia watoto wengi zaidi na kutoa fursa kwa kizazi kijacho kupata lishe bora kupitia matumizi ya maziwa.
“Tunapaswa kuongeza idadi ya shule zinazotekeleza mpango wa ununuzi na unywaji wa maziwa shuleni ili watoto wengi zaidi waweze kunufaika,” amesema Dkt. Nguvila.
Amesema elimu ya lishe inapaswa kuanzia katika ngazi ya familia, kwa kuwa wazazi wana nafasi kubwa katika kujenga tabia za ulaji na unywaji zinazoweza kuendelea kuwa sehemu ya maisha ya mtoto hadi ukubwani.
MAZIWA YAANZE UTOTONI
Amesema kuwazoesha watoto kutumia maziwa ni sehemu ya kujenga msingi wa lishe bora, huku akieleza kuwa familia zina nafasi kubwa katika kuhakikisha watoto wanapata maziwa na bidhaa zake kwa kiwango kinachofaa.
Prof. Msalya amesema suala la unywaji wa maziwa halipaswi kuachwa kuwa jukumu la shule pekee, bali linahitaji ushiriki wa wazazi na jamii nzima.
Amesema mazingira ya nyumbani yana mchango mkubwa katika kujenga tabia za mtoto, hivyo juhudi za kuongeza unywaji wa maziwa shuleni zinapaswa kuambatana na elimu kwa wazazi na jamii.
MTAALAMU ATOA MSUKUMO WA LISHE
Kwa upande wake, mtaalamu wa lishe, Dkt. Mackrina Nombo, amesema maziwa yana virutubisho muhimu vinavyohitajika katika ukuaji na ustawi wa watoto.
Amesema ni muhimu jamii kuendelea kuzingatia lishe bora baada ya mtoto kumaliza kipindi cha kunyonyesha, kwa kuhakikisha anapata mlo wenye mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali kulingana na mahitaji yake.
Dkt. Nombo amesema maziwa yanaweza kuwa sehemu ya mlo unaosaidia ukuaji wa mtoto, huku akisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kupata elimu sahihi kuhusu lishe na mahitaji ya watoto katika hatua mbalimbali za ukuaji.
MPANGO WA MIAKA 10
Mpango wa ununuzi na unywaji wa maziwa shuleni ulianza mwaka 2024 na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10, ukiwa na malengo ya kuboresha lishe ya watoto, kuongeza matumizi ya maziwa na wakati huo huo kuimarisha tasnia ya maziwa nchini.
Mpango huo unalenga kuunganisha mahitaji ya watoto shuleni na uzalishaji wa maziwa nchini, hatua inayoweza kuongeza soko la bidhaa za maziwa na kutoa nafasi kwa wazalishaji kuongeza uzalishaji.
Wadau wamesisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, shule, wazazi, wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa za maziwa ili kuhakikisha maziwa yanawafikia watoto kwa usalama na kwa utaratibu unaoeleweka.
Kwa upande wa jamii, msisitizo umetolewa juu ya umuhimu wa kuanza kuwazoesha watoto maziwa wakiwa wadogo ili kujenga utamaduni wa matumizi ya bidhaa hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya lishe ya kila siku.
Kongamano hilo limekuwa sehemu ya maandalizi ya kuelekea Siku ya Unywaji wa Maziwa Shuleni, huku wadau wakitumia jukwaa hilo kujadili namna ya kuongeza matumizi ya maziwa, kuboresha lishe ya watoto na kuimarisha sekta ya maziwa nchini.
Ends











إرسال تعليق