Breaking🔥

TOIMA AWAONYA WANAONYEMELEA NAFASI ZA UONGOZI CCM MANYARA,APIGA MKWARA MAKUNDI NA MATUMIZI YA MITANDAO YASIOFAA

TOIMA AWAONYA WANAONYEMELEA NAFASI ZA UONGOZI CCM MANYARA

....Asema muda wa uchaguzi haujafika, ataka viongozi kuheshimiwa na taratibu za chama kuzingatiwa

Na Joseph Ngilisho | MANYARA

MANYARA. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Peter Toima, ametoa onyo kali kwa viongozi na wanachama wanaoanza kujipanga na kunyemelea nafasi za uongozi wa chama hicho, akisema hatua hiyo inakiuka taratibu na inaweza kuvuruga utulivu ndani ya chama.

Toima amesema uchaguzi wa CCM tayari ulifanyika na viongozi walipatikana kwa mujibu wa taratibu, hivyo kwa sasa hakuna sababu kwa mwanachama au kiongozi kuanza kampeni za chinichini kwa lengo la kuchukua nafasi ya kiongozi aliye madarakani.

Alisema hadi sasa hakuna tamko wala maelekezo rasmi kutoka CCM yanayotangaza kuanza kwa uchaguzi mwingine, hivyo wanachama wanapaswa kuendelea kutekeleza majukumu waliyopewa badala ya kujihusisha na harakati za kutafuta nafasi za wengine.

“Uchaguzi ulikwisha na viongozi walipatikana. Hakuna tamko lingine lolote au maelekezo kuhusu uchaguzi mwingine. Wakati haujafika, watu waache kutafuta nafasi, waache kunyemelea. Huo sio utaratibu na unamkwaza kiongozi aliyepo madarakani,” alisema Toima.

Mwenyekiti huyo alisema tabia ya baadhi ya wanachama kuanza kujipanga mapema kwa ajili ya nafasi za uongozi, ikiwamo kuwanyemelea viongozi waliopo madarakani, haipaswi kuvumiliwa kwa kuwa inaweza kuzaa migogoro, makundi na mpasuko ndani ya chama.

Alisema kila mwanachama anapaswa kuheshimu nafasi za viongozi waliopo na kusubiri muda sahihi utakapotangazwa na chama, huku akisisitiza kuwa uongozi wa CCM haupaswi kugeuzwa kuwa mashindano ya mapema yasiyo na msingi wa taratibu rasmi.

Toima alisema CCM Mkoa wa Manyara itafuatilia mienendo ya watu wanaoanza kulenga majimbo au nafasi za viongozi wenzao, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda nidhamu na utulivu wa chama.

“Tuweke mafaili kwa watu wanaonyemelea majimbo ya mwenzake. Tuweke utulivu kwenye mkoa. Tuheshimu taratibu za chama. Kila mmoja afanye kazi yake,” 

Alisema katika kipindi chake cha uongozi hatakubali vitendo vinavyokiuka taratibu za CCM, akiwataka viongozi na wanachama kuacha kujenga makundi yanayolenga kushindana au kudhoofisha viongozi waliopo madarakani.

“Kila mmoja afanye kazi yake kwa nafasi aliyopewa. Tuheshimiane na tuheshimu viongozi waliopo madarakani,” alisema.

Aidha, Toima alisisitiza umuhimu wa kuheshimu muundo wa uongozi wa CCM, akiwataka wanachama wanaohitaji huduma au kushughulikia masuala ya chama kufuata ngazi za uongozi zilizowekwa badala ya kuruka mamlaka.

Alisema kuheshimu mfumo huo kutasaidia kuimarisha nidhamu, mshikamano na ufanisi wa chama, huku viongozi wakitakiwa kutekeleza wajibu wao bila kuingiliwa na harakati za watu wanaotafuta nafasi zao kabla ya wakati.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Manyara katika Wilaya ya Babati, ikiwa ni sehemu ya ziara inayofanyika katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Ziara hiyo inatoa nafasi kwa viongozi wa chama kufuatilia utekelezaji wa shughuli za CCM, kusikiliza changamoto za wanachama na kuhimiza nidhamu, mshikamano na utekelezaji wa majukumu ya chama katika ngazi mbalimbali.

Ends

Post a Comment

Previous Post Next Post