Breaking🔥

RC BATILDA: RUSHWA IKOMESHWE KABLA WATOTO HAWAJAJIFUNZA KUIPENDA.

 RC BATILDA: RUSHWA IKOMESHWE KABLA WATOTO HAWAJAJIFUNZA KUIPENDA. 

Asema elimu ya kupinga rushwa ianze darasa la tatu, wazazi na walimu washirikishwe kujenga kizazi cha waadilifu

Na Hadija Bagasha Tanga, 

SERIKALI mkoani Tanga imetaka mapambano dhidi ya rushwa yaanze kwenye ngazi ya chini kabisa ya elimu, ikiwamo shule za msingi, kwa kuwafundisha watoto madhara ya rushwa na kuwajengea misingi ya uadilifu, uaminifu, uwajibikaji na uzalendo tangu wakiwa wadogo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi kitakachokataa rushwa kama sehemu ya maisha yake na badala yake kusimamia haki, ukweli na maendeleo ya taifa.



Amesema elimu hiyo inapaswa kuanza mapema, akipendekeza wanafunzi waanze kufundishwa masuala ya kupinga rushwa kuanzia darasa la tatu, ili misingi ya maadili ijengwe kabla ya mtoto hajakua na kuingia katika mazingira mapana zaidi ya kijamii.

Dk. Burian alitoa kauli hiyo wakati wa fainali ya mashindano ya Chemsha Bongo Zuia Rushwa 2026 mkoani Tanga, yaliyofanyika katika Shule ya Ufundi Tanga (Tanga Technical Secondary School) aliyewakilishwa katika hafla hiyo na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Tanga, Emanuel Kisongo. 

Alisema watoto wana nafasi kubwa katika mapambano ya muda mrefu dhidi ya rushwa kwa kuwa elimu wanayoipata wakiwa wadogo inaweza kuwa sehemu ya misingi ya maisha yao ya baadaye.

Kwa mujibu wa Dkt Burian, kuwafundisha watoto kuhusu rushwa hakupaswi kuishia katika kutaja maana yake, bali wanapaswa kuelewa madhara yake kwa jamii, uchumi, huduma za kijamii na maendeleo ya nchi.

“Kama mlivyowasikia wanafunzi wakijieleza, wameonesha namna rushwa inavyodumaza maendeleo. Inaweza kusababisha kujengwa kwa madaraja mabovu kwa sababu ya kumpa kazi mkandarasi asiye na sifa. Mwisho serikali hudhani imetekeleza maendeleo, kumbe ni maendeleo ya magumashi,” alisema.

Dk. Burian, ambaye aliwakilishwa katika hafla hiyo na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Tanga, Emanuel Kisongo, 

alisema walimu wana wajibu mkubwa wa kuwa vielelezo vya maadili kwa wanafunzi.

Alisema mwalimu anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na mtoto katika uadilifu, uwajibikaji na uzingatiaji wa sheria, huku akisisitiza umuhimu wa kuwafundisha wanafunzi athari za rushwa katika maisha ya kila siku.

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo programu za uhamasishaji dhidi ya rushwa zikilenga zaidi kuwafikia wananchi katika ngazi mbalimbali, huku elimu kwa watoto ikionekana kuwa sehemu muhimu ya kujenga utamaduni wa kupinga vitendo hivyo kwa muda mrefu.

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwata, alisema mashindano ya Chemsha Bongo Zuia Rushwa 2026 ni sehemu ya mkakati wa kujenga kizazi chenye uadilifu kupitia elimu.

Alisema lengo si kuwafanya wanafunzi wajue tu maana ya rushwa, bali kuwajenga kuwa raia watakaoweza kutambua, kukataa na kupinga vitendo vya rushwa wanapokutana navyo katika jamii.

“Tunataka kujenga kizazi kitakachokuwa sehemu ya suluhisho la tatizo la rushwa badala ya kuwa sehemu ya tatizo. Vitendo vina nguvu kubwa katika kujenga maadili kuliko maneno pekee,” alisema. 

Ndwata alisema kuanzishwa kwa Klabu za Wapinga Rushwa katika shule za msingi kumeanza kuleta matokeo chanya, akieleza kuwa wanafunzi wamekuwa na uwezo wa kujadiliana na hata kusahihishana kuhusu masuala yanayohusu rushwa.

Alisema hali hiyo ni ishara kwamba wanafunzi wameanza kuielewa ajenda ya kupinga rushwa na wanaweza kuwa mabalozi wa ujumbe huo katika shule, familia na jamii kwa ujumla.

Ndwata aliwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto na kushirikiana na shule pamoja na wadau wengine kuhakikisha elimu ya kupinga rushwa haiishii darasani.

Alisema familia ina nafasi kubwa katika kujenga au kuvunja misingi ya maadili ya mtoto, hivyo wazazi wanapaswa kuwa sehemu ya juhudi za kuwafundisha watoto umuhimu wa uaminifu, haki, uwajibikaji na kuheshimu sheria.

Mashindano yaibua mabalozi wa rushwa

Katika fainali hiyo, Shule ya Msingi Kombezi iliibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia kombe kubwa pamoja na Sh200,000.

Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Msingi Bombo ilishika nafasi ya pili na kupata kombe dogo pamoja na Sh150,000, huku Shule ya Msingi Chumbageni ikiibuka ya tatu na kujishindia ngao ya glasi pamoja na Sh100,000.

Nafasi ya nne ilichukuliwa na Klabu ya Wapinga Rushwa ya Shule ya Msingi Nguvumali iliyopata ngao ya plastiki pamoja na Sh50,000.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkwakwani alisema kuanzishwa kwa klabu hizo kumesaidia kuongeza uadilifu na ujasiri kwa wanafunzi, huku kukiwajengea msingi wa kuwa raia wema watakaoheshimu sheria na kutenda haki.

Naye mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kisosora, Mariam Juma, alisema klabu hizo zimekuwa nyenzo muhimu katika kuwaelimisha wanafunzi kuhusu madhara ya rushwa kwa jamii na taifa.

“Ni muhimu wigo wa klabu hizi ukaongezwa ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na elimu hii na ujumbe uwafikie wote,” alisema.

Mwisho.

Post a Comment

Previous Post Next Post