PAC YAANZA KUCHAMBUA HESABU ZA TANAPA ZA MWAKA 2024/2025
Na Joseph Ngilisho | DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeanza kuchambua taarifa ya hesabu za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.Kikao hicho kiliongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa PAC, Mhe. Aeshi Hilaly (Mb), na kufanyika jana, Agosti 18, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma.
Katika kikao hicho, kamati ilipitia na kuchambua kwa kina taarifa ya hesabu za TANAPA, ikilenga kupata ufafanuzi kuhusu mwenendo wa matumizi na usimamizi wa fedha za shirika hilo, kwa kuzingatia hoja na mapendekezo yaliyotolewa katika ukaguzi wa CAG.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, pamoja na maafisa kutoka TANAPA wakiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Massana Mwishawa.
Aidha, maafisa kutoka Ofisi ya CAG, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) na Wizara ya Fedha walishiriki katika kikao hicho, huku wakitoa ufafanuzi na taarifa zinazohusiana na masuala yaliyokuwa yakichambuliwa na kamati.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la PAC la kuisimamia Serikali katika matumizi na usimamizi wa fedha za umma, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yanayotokana na ripoti za CAG.




Post a Comment