MAVUNDE AITAKA FLANONE KUONGEZA UTAFITI UZALISHAJI TANZANITE, AZINDUA KOFIA ZA KUDHIBITI WIZI TANZANITE
Na Joseph Ngilisho |MERERANI, MANYARA
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameitaka kampuni ya Flanone Mining Ltd, inayochimba madini ya Tanzanite katika Kitalu C eneo la Mererani, kuongeza utafiti wa kina ili kubaini maeneo mapya yenye madini hayo na kuongeza uzalishaji.
Mavunde alitoa kauli hiyo leo Agosti 24,2026 wakati alipotembelea mgodi huo wilayani Simanjiro -Manyara na kukagua shughuli za uchimbaji, huku akisisitiza umuhimu wa kampuni kuongeza uwekezaji katika utafiti na kutumia teknolojia za kisasa katika uchimbaji wa Tanzanite.Alisema utafiti wa kina ni muhimu kwa kuwa bado kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa rasilimali zaidi ya Tanzanite katika eneo la Mererani, hivyo kampuni zinapaswa kutumia teknolojia na mbinu bora kubaini maeneo yenye madini na kuongeza uzalishaji.
“Lazima tuongeze utafiti katika maeneo yetu ya Tanzania. Imani yangu ni kwamba tukifanya utafiti wa kutosha katika eneo hili la Tanzanite, tunaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema Mavunde.
Wakati huo huo, Mavunde amezindua matumizi ya kofia ngumu maalumu zenye teknolojia ya kusaidia kuona mbali ndani ya migodi, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa wachimbaji pamoja na kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini ya Tanzanite.
Kofia hizo zimezinduliwa katika mgodi wa Flanone Mining Ltd kama sehemu ya matumizi ya teknolojia katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za uchimbaji na ulinzi wa rasilimali za madini.
Mavunde alisema matumizi ya teknolojia hiyo yataisaidia Serikali na kampuni za uchimbaji kuongeza udhibiti ndani ya migodi, kufuatilia shughuli za uchimbaji na kupunguza mianya inayoweza kutumiwa na watu kufanya vitendo vya wizi wa madini.
Alisema Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia katika sekta ya madini ili kuongeza ufanisi, usalama na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana nchini zinawanufaisha Watanzania.
Mavunde pia alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika kutatua changamoto zinazowakabili, huku akiwataka kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia sheria, usalama na maslahi ya Taifa.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha Tanzania inaongeza thamani ya madini yake, hususan Tanzanite, na kupata manufaa makubwa zaidi kiuchumi kutokana na rasilimali hiyo ya kipekee.
Ends..





Post a Comment