LUKUMAY: VIFO VYA MAMA VYASHUKA, SERIKALI YAWEKA LENGO LA CHINI YA 70
Na Joseph Ngilisho
DODOMA. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amesema mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi yanapaswa kuambatana na ufuatiliaji madhubuti wa utekelezaji wa mikakati ya Serikali ili kuhakikisha huduma bora za afya ya uzazi, mama na mtoto zinawafikia wananchi kwa wakati.
Dkt. Lukumay ameyasema hayo jana, Agosti 11, 2026, jijini Dodoma, baada ya Kamati yake kupokea na kujadili taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu hali ya huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Taarifa hiyo iliwasilishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Frolence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa mbele ya Kamati, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi kimeshuka kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 hadi vifo 104 mwaka 2022, huku Serikali ikiweka lengo la kukifikisha chini ya vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Lukumay amesisitiza umuhimu wa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mikakati hiyo, akieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kuchochea juhudi zaidi katika kuboresha huduma kwa mama na mtoto.
WANAWAKE 93% WAJIFUNGUA VITUONI
Taarifa ya Wizara imeonyesha pia kuwa idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka asilimia 81 mwaka 2021 hadi asilimia 93 mwaka 2026.
Aidha, mahudhurio ya kwanza ya kliniki kwa wajawazito kabla ya kufikisha wiki 12 yameongezeka kutoka asilimia 37 hadi asilimia 60, hatua inayolenga kuwezesha huduma na uchunguzi wa mapema kwa wajawazito.
NCU ZAFIKIA 438
Katika kuimarisha huduma kwa watoto wachanga, Serikali imeongeza idadi ya Wodi Maalum za Watoto Wachanga (NCU) kutoka 362 hadi 438 katika mwaka 2025/2026.
Vilevile, ujenzi wa NCU 35 za kisasa unaendelea katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 15 na Halmashauri 20.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa vituo vya afya kutoa huduma maalumu kwa watoto wachanga, hususan wanaohitaji uangalizi wa karibu na matibabu baada ya kuzaliwa.
M-MAMA, AMBULANSI 613
Kamati pia imeelezwa kuhusu hatua za kuimarisha mfumo wa M-MAMA, ambao unasaidia kurahisisha usafirishaji wa wajawazito na watoto wanaohitaji huduma za dharura.
Serikali imefanikiwa kununua ambulansi 613 kwa ajili ya kuwezesha usafirishaji wa haraka wa wagonjwa hao, huku mfumo huo ukiendelea kutumika Tanzania Bara na Zanzibar.
Dkt. Lukumay amesema Kamati itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mikakati hiyo na kutoa ushauri unaolenga kuimarisha zaidi huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wakati na kwa ubora katika ngazi zote za utoaji wa huduma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Taifa kufikia lengo la kupunguza zaidi vifo vya mama na watoto ifikapo mwaka 2030.




Post a Comment