WAZIRI WA FEDHA AAMURU DORIA KALI HOROHORO, APIGA VITA MAGENDO KULINDA MAPATO NA USALAMA WA TAIFA

 WAZIRI WA FEDHA AAMURU DORIA KALI HOROHORO, APIGA VITA MAGENDO KULINDA MAPATO NA USALAMA WA TAIFA

Na Hadija Bagasha, Tanga


SERIKALI imeagiza kuimarishwa mara moja kwa doria na operesheni maalumu za kukabiliana na biashara ya magendo katika mpaka wa Horohoro, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, ikisisitiza kuwa vitendo hivyo vinasababisha upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali, vinahatarisha usalama wa Taifa na kudhoofisha ukuaji wa uchumi.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Forodha cha Horohoro kukagua mwenendo wa ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa biashara ya mpakani na utekelezaji wa majukumu ya forodha katika mpaka wa Tanzania na Kenya.

Akizungumza na viongozi wa Serikali, maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, Waziri Omar alisema mapambano dhidi ya magendo yanapaswa kupewa uzito wa kipekee kwa kuwa yanahusu ulinzi wa uchumi wa Taifa, usalama wa wananchi na upatikanaji wa takwimu sahihi za biashara zinazotumika kupanga maendeleo ya nchi.

Alisisitiza kuwa maofisa wa forodha hawapaswi kujikita katika ukusanyaji wa mapato pekee, bali wanapaswa kuhakikisha bidhaa zilizopigwa marufuku haziingii nchini na sheria zote za forodha zinatekelezwa kikamilifu.

"Tusipotekeleza jukumu hili ipasavyo tunaweza kulisababishia Taifa madhara makubwa. Sisi maofisa wa forodha hatuna jukumu la kukusanya mapato pekee, bali pia kuhakikisha bidhaa zilizopigwa marufuku haziingii nchini. Usalama wa Taifa ni jambo ambalo hatuwezi kulifumbia macho," alisema Waziri Omar.

Aliongeza kuwa Serikali haiwezi kupanga sera madhubuti za maendeleo bila kuwa na takwimu sahihi za biashara, hivyo akaitaka TRA kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama katika ngazi zote ili kuziba mianya ya magendo na kuongeza ufanisi wa usimamizi wa mipaka.

Katika ziara hiyo, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Horohoro, Shadrack Mbonea, alisema licha ya kituo hicho kuendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, bado kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mashine ya kisasa ya kukagua mizigo (Scanner), hali inayochelewesha ukaguzi na kupunguza ufanisi wa huduma.

Alieleza kuwa Serikali imepanga kununua mashine hiyo katika miaka ya fedha 2026/2027 na 2027/2028, hatua itakayorahisisha ukaguzi wa mizigo, kuongeza kasi ya utoaji wa huduma na kuimarisha udhibiti wa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini.

Mbonea pia aliiomba Serikali kukipatia kituo hicho huduma ya umeme wa uhakika kupitia Dedicated Line, akibainisha kuwa kukatika kwa umeme mara kwa mara kutokana na uchakavu wa miundombinu kumeendelea kuathiri utendaji wa mifumo ya forodha na utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, alisema changamoto ya ukosefu wa barabara bora kandokando ya mpaka imekuwa ikitoa mwanya kwa wafanyabiashara haramu kutumia njia zisizo rasmi maarufu kama njia za panya kuingiza bidhaa za magendo kutoka Kenya.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo utarahisisha doria za vyombo vya ulinzi na usalama, kufunga njia za magendo na kuimarisha usalama wa mpaka, huku ukiwezesha Serikali kuongeza mapato yatokanayo na biashara rasmi.

Hatua ya Waziri wa Fedha kuagiza kuimarishwa kwa doria katika mpaka wa Horohoro ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha ulinzi wa mipaka, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, kudhibiti biashara haramu na kuhakikisha shughuli zote za biashara ya kimataifa zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Post a Comment

أحدث أقدم