WANAFUNZI ENGOSENGIU WANUFAIKA NA KISIMA CHA MAJI SAFI, BUSTANI YA MBOGA NA UWANJA WA MICHEZO WA SH. MILIONI 60
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Engosengiu, Katika jiji la Arusha pamoja na jamii inayozunguka eneo hilo wameondokana na changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kunufaika na mradi wa kisima cha kisasa kinachotumia nishati ya jua, uliojengwa na shirika lisilo la kiserikali la WorldServe International Tanzania.
Mradi huo ni sehemu ya miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 60 iliyotekelezwa na shirika hilo katika shule hiyo, ikiwemo mfumo wa kisasa wa umwagiliaji wa bustani ya mbogamboga na ujenzi wa uwanja wa mpira wa kikapu, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia, afya, lishe na michezo kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi miradi hiyo leo Jumanne Julai 14,2026, Mwakilishi wa WorldServe International Tanzania, Joel Allan, alisema shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi ya kusaidia jamii katika maeneo mbalimbali nchini, likijikita zaidi katika huduma za maji safi, afya, michezo na lishe bora.
Alisema miradi hiyo imefadhiliwa na wadau wa shirika hilo wanaofahamika kama UTU, ambao wamekuwa wakishirikiana na WorldServe katika kusaidia jamii zenye uhitaji.
"Tumekuja Engosengiu kuzindua miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na wadau wetu wa UTU kwa lengo la kuboresha maisha ya wanafunzi na jamii kwa ujumla," alisema Joel.
Alieleza kuwa kisima hicho kinachotumia mfumo wa pampu ya nishati ya jua kitaiwezesha shule pamoja na wananchi wanaoizunguka kupata maji kwa urahisi na kwa uhakika, huku maji hayo yakiwa yameondolewa madini ya fluoride ambayo yamekuwa yakihusishwa na changamoto za afya katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Arusha.
Aidha, alisema shirika hilo limejenga bustani ya kisasa ya mbogamboga inayotumia mfumo wa umwagiliaji wa matone (drip irrigation), ambao husaidia kutumia maji kwa ufanisi na kuongeza uzalishaji wa mazao.
"Bustani hii itasaidia kuboresha lishe ya wanafunzi kwa kuwapatia mboga za majani, huku mazao yatakayozalishwa kwa ziada yakiuzwa ili kusaidia kuendeleza mradi," alisema.
Mbali na huduma za maji na lishe, WorldServe International Tanzania pia imejenga uwanja wa mpira wa kikapu katika shule hiyo, hatua inayolenga kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo.
WANAFUNZI WAONDOKANA NA USUMBUFU WA KUBEBA VIDUMU VYA MAJI
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Engosengiu, Ali Ramadhani, alisema mradi huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa wanafunzi na jamii kwa kuwa umeondoa changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikikabili shule hiyo.
Alisema kabla ya kupatikana kwa kisima hicho, wanafunzi walikuwa wakikumbana na changamoto ya kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya shule na kumwagilia bustani, hali iliyosababisha baadhi yao kutumia muda mwingi kubeba vidumu vya maji badala ya kujikita katika masomo.
"Maji haya yatasaidia sana shule yetu. Tutakuwa na uhakika wa maji kwa matumizi ya kila siku, kumwagilia bustani ya mbogamboga na kuwaondolea wanafunzi usumbufu wa kutafuta maji," alisema.
Aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kupitia uboreshaji wa miundombinu ya shule na utoaji wa fedha za elimu bila malipo.
Alisema kwa mwaka huu wa fedha shule hiyo imepokea fedha zilizowezesha ukarabati wa madarasa mawili, huku ikiendelea kuwa na mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi 173 waliopo shuleni.
Pia alisema kupitia ushirikiano kati ya uongozi wa shule, Serikali ya mtaa na wazazi, wanafunzi wameendelea kupata chakula cha mchana, jambo linalosaidia kuongeza mahudhurio na kuboresha ufaulu.
DIWANI SINONI AWATAKA WANANCHI KULINDA MRADI
Diwani wa Kata ya Sinoni, Peter Inyasi, ameishukuru WorldServe International Tanzania kwa kutekeleza mradi huo, akisema umeleta matumaini mapya kwa wananchi na wanafunzi wa eneo hilo.
Alisema kwa muda mrefu Kata ya Sinoni, hususan eneo la Engosengiu, lilikuwa likikabiliwa na changamoto ya maji ambayo iliathiri shughuli mbalimbali za kijamii na mazingira ya kujifunzia.
"Kwa muda mrefu tumekuwa na changamoto kubwa ya maji katika Kata ya Sinoni. Lakini leo tunashukuru tumepata wafadhili ambao wameweza kuchimba kisima hiki kirefu na kupata maji ambayo hayana fluoride, hivyo ni salama kwa wananchi kuyatumia," alisema.
Diwani Inyasi alisema mradi huo utawasaidia wanafunzi kuondokana na tabia ya kubeba vidumu vya maji kutoka majumbani, huku ukiwezesha shule kuendeleza bustani za mbogamboga zitakazosaidia kuongeza lishe bora kwa wanafunzi.
Aliwataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
DIWANI SOPHIA MWIDANI AIPONGEZA WORLDSERVE
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu, Sophia Mwidani, ameipongeza WorldServe International Tanzania kwa utekelezaji wa miradi hiyo akisema imeongeza matumaini kwa wanafunzi na jamii inayozunguka shule hiyo.
Amesema ujenzi wa uwanja wa michezo utawapa wanafunzi nafasi ya kukuza vipaji vyao, hasa katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea na maandalizi kuelekea mashindano ya AFCON 2027.
"Tunashukuru sana kwa mradi huu wa uwanja wa mpira kwa ajili ya watoto wetu wa Shule ya Engosengiu. Hii ni hatua kubwa katika kuboresha mazingira ya watoto wetu na kuwasaidia kuendeleza vipaji vyao," amesema Mwidani.
Aidha, amesema mradi wa maji utasaidia wanafunzi na wananchi kwa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji, huku ukirahisisha shughuli za shule ikiwemo kumwagilia bustani za mbogamboga na matumizi mengine ya kila siku.
Ameahidi kuwa viongozi wa eneo hilo wataendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha miradi hiyo inalindwa na kutumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.
Miradi hiyo ya WorldServe International Tanzania inatarajiwa kuwa chachu ya kuboresha afya, lishe, elimu na michezo kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Engosengiu pamoja na jamii inayozunguka eneo hilo.

















Post a Comment