SERIKALI YAAHIDI SH. MILIONI 750 KUKAMILISHA KITUO CHA AFYA MAWENI
Na Hadija Bagasha, Tanga
SERIKALI imeahidi kutoa Shilingi milioni 750 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyobaki katika Kituo cha Afya cha Maweni, jijini Tanga, hatua inayotarajiwa kuboresha huduma za afya kwa zaidi ya wakazi 40,000 wa Kata ya Maweni na maeneo jirani.
Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Kituo cha Afya cha Maweni na mradi wa mabweni katika Shule ya Sekondari Usagara.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Balozi Omar alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan katika sekta za afya, elimu na miundombinu, ili kuhakikisha huduma za msingi zinawafikia wananchi kwa ufanisi.
Alisema Mkoa wa Tanga umeendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika mwaka wa fedha 2025/2026, hali inayoonyesha dhamira ya Serikali ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Kwa mwaka huu wa fedha uliopita, Mkoa wa Tanga ulipangiwa kutumia Shilingi bilioni 528.1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, na Serikali tayari imetoa Shilingi bilioni 487.5, sawa na zaidi ya asilimia 92 ya fedha zote zilizopangwa," alisema.
Waziri huyo pia aliipongeza Bandari ya Tanga kwa usimamizi mzuri wa fedha za umma na mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa mapato, akisema uwekezaji wa Serikali unaendelea kuzaa matunda.
Alieleza kuwa Serikali imewekeza Shilingi bilioni 429.1 katika uboreshaji wa Bandari ya Tanga, huku bandari hiyo ikikusanya mapato ya Shilingi bilioni 436, kiwango kilichovuka thamani ya uwekezaji huo.
"Mmefanya kazi nzuri. Serikali imewekeza, fedha zimerudi na bado mmevuka malengo ya makusanyo. Huu ni mfano wa matumizi sahihi ya fedha za umma," alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Jiji la Tanga, Dkt. Stephen Mwandambo, alisema Kituo cha Afya cha Maweni kitakapokamilika kitatoa huduma kwa zaidi ya wakazi 40,740 wa Kata ya Maweni ambao kwa muda mrefu walikuwa wakisafiri umbali mrefu kupata huduma za afya, hususan huduma za uzazi na matibabu ya dharura.
Alisema Halmashauri ya Jiji la Tanga tayari imetenga Shilingi milioni 75 katika mwaka wa fedha ujao kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya majengo muhimu, yakiwemo kichomea taka, jengo la upasuaji na wodi ya wazazi.
Hata hivyo, alisema ili kituo hicho kifikie hadhi ya kituo cha afya kamili bado kinahitaji kujengwa majengo manane muhimu, ambayo ni jengo la utawala, jengo la mama na mtoto, wodi za wagonjwa, jengo la X-ray, nyumba za watumishi, jengo la kuhifadhia maiti, njia za kupitishia wagonjwa (walkways) pamoja na uzio wa usalama.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, alisema Serikali imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 357 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji la Tanga kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Alisema kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 1.8 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekta ya afya, huku Hospitali ya Wilaya ya Masiwani ikipokea Shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kuimarisha huduma za matibabu. Aidha, Shilingi milioni 548 zimetumika kujenga nyumba za watumishi na kuboresha vituo vya afya vya Mleni, Maweni, Pande na Chongoleani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, Meja (Mstaafu) Hamis Mkoba, aliiomba Serikali kusaidia kupatikana kwa Shilingi bilioni 24.7 za mapato ya kodi ambazo zimekwama katika baadhi ya taasisi tangu mwaka 2022, akisema fedha hizo zingechangia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Jiji la Tanga.
Naye mkazi wa Kata ya Maweni, Juma Abdala, alisema kukamilika kwa Kituo cha Afya cha Maweni kutapunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya na kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu karibu na makazi yao.
"Ujenzi wa kituo hiki tayari umeleta nafuu kubwa kwa wananchi. Serikali ikitekeleza ahadi yake ya kutoa fedha za kukamilisha majengo yaliyobaki, huduma za afya zitaboreshwa zaidi na wananchi watanufaika kwa kiwango kikubwa," alisema.
Ends


Post a Comment