WAKAZI OLORIEN WAMSIMAMISHA MBUNGE LUKUMAY WAKILALAMIKIA MAFURIKO YA MAJI YALIYOELEKEZWA KWENYE MAKAZI YAO YAKIWATESA KWA MIAKA 16,MBUNGE ATOA MAELEKEZO

WAKAZI WAMSIMAMISHA LUKUMAY, WALIA MAFURIKO YA MIAKA 16

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU


WAKAZI zaidi ya 100 wa Kijiji cha Olorien, Kata ya Olorien, Halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru, walimsimamisha Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, akiwa njiani kwenda Hospitali ya Seliani, wakimweleza kilio chao cha miaka 16 kuhusu mafuriko yanayodaiwa kusababishwa na maji ya mvua kuelekezwa kwenye makazi yao.

Wananchi hao walidai zaidi ya familia 20 zimekuwa zikiathirika kila msimu wa mvua kutokana na maji kuelekezwa katika makazi yao, hali iliyosababisha uharibifu wa nyumba, vyoo, visima vya maji, barabara na miundombinu mingine, huku watoto wakishindwa kwenda shule na wagonjwa pamoja na wajawazito kushindwa kufikishwa hospitalini.

Walisema licha ya kuwasilisha malalamiko yao kwa viongozi wa kijiji, wilaya na mkoa kwa zaidi ya miaka 16, bado hawajapata suluhisho la kudumu, huku wakihofia kuwa mradi wa barabara ya lami ya Mianzini–Ngaramtoni unaweza kuongeza athari hizo iwapo mifereji ya maji haitajengwa kwa kuzingatia mazingira ya eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mzee Abel Moshi alisema kila mvua inaponyesha maji yote hukusanyika katika makazi yao na kusababisha hasara kubwa.

"Tumekuwa tukilalamika kwa zaidi ya miaka 16 lakini hakuna hatua za kudumu zilizochukuliwa. Maji yote yanaelekezwa kwenye makazi yetu na kutusababishia hasara kubwa kila msimu wa mvua," alisema.

Balozi wa eneo hilo, Ortensia Moshi, alisema mafuriko hayo yamegeuka janga la kudumu, huku baadhi ya nyumba zikiporomoka na familia nyingi kubaki bila vyoo na visima salama.

"Mvua ikinyesha watoto hawaendi shule, wananchi hawaendi kazini na baadhi ya nyumba zimeporomoka. Tunaomba Serikali ijenge mfumo wa mifereji utakaoyaelekeza maji mtoni badala ya kuishia kwenye makazi yetu," alisema.


Naye Venosa Saringo alisema ujio wa Mbunge Lukumay umewapa matumaini mapya baada ya kusikiliza kero yao, akimtaka kuhakikisha wahandisi wa TANROADS wanarekebisha mfumo wa mifereji ili kuzuia maji kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Dkt. Lukumay alimwelekeza Diwani wa Kata ya Olorien, Hendry Sikoi, kuwasilisha rasmi tatizo hilo kwa TANROADS Mkoa wa Arusha ili wahandisi wafike kufanya tathmini na kutoa suluhisho la kudumu.

Mbunge huyo alisema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imetoa fedha zote kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa barabara ya Mianzini–Ngaramtoni wenye urefu wa kilomita 18, ikiwemo fidia ya takribani Sh bilioni 3.4 kwa wananchi 552 walioathiriwa na mradi huo.

Alifafanua kuwa mitaro ya kupitisha maji ya mafuriko itajengwa baada ya kukamilika kwa kazi ya uwekaji wa lami ili kuepusha kuharibika kutokana na matumizi ya mitambo mizito inayotumika katika ujenzi.

"Mitambo inayoweka lami ni mizito. Tukijenga mitaro kabla ya lami inaweza kuharibika. Ndiyo maana mitaro sanifu itajengwa baada ya uwekaji wa lami kukamilika ili iwe ya kudumu na iweze kupitisha maji kwa usalama," alisema.

Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na wahandisi wa TANROADS kwa kuwaonyesha maeneo yote yenye changamoto za mafuriko badala ya kulaumu, akisema ushirikiano huo utasaidia kupata suluhisho la kudumu.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Olorien, Hendry Sikoi, alisema jiografia ya eneo hilo husababisha maji kutoka maeneo ya juu kuelekea Olorien, hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa barabara, visima vya maji na makazi ya wananchi.

Alitoa wito kwa Serikali kuhakikisha barabara zote zinazojengwa katika kata hiyo zinakuwa na mifereji ya kisasa ya kupitisha maji ili kuondoa adha ya mafuriko ambayo imekuwa ikiwasumbua wananchi kwa zaidi ya miaka 16.

ENDS

Post a Comment

Previous Post Next Post